Na Mwandishi Wetu, Tarime
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itahakikisha inajenga na kukamilisha kwa kiwango cha lami miradi yote viporo ya miundombinu ya barabara na madaraja nchini.
Akizungumza na wananchi wa Isenye mkoani Mara baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara ya Tarime–Mugumu (km 87.14) na Sanzate–Natta (km 40), Waziri huyo alisema hatua iliyofikiwa katika mradi wa Sanzate–Natta ni kubwa, hivyo kuachwa kwake kutasababisha hasara kwa fedha za walipa kodi.
“Hakuna mradi kiporo utakaobakia; ni lazima yote ikamilike. Huu ni mradi kiporo, hivyo mkandarasi atarejea kuendelea na kazi. Naomba muendelee kuamini kwamba Serikali haiwezi kupoteza fedha hizi,” alisema Ulega.
Aidha, alifafanua kuwa ukamilishaji wa barabara hiyo utaambatana na uwekaji wa taa za barabarani ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao usiku na mchana.
Waziri huyo pia alieleza umuhimu wa barabara katika kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii kama masoko, shule na hospitali, na kusisitiza kuwa miundombinu hiyo itachochea maendeleo ya wananchi.
Katika hatua nyingine, akiwa Tarime Mjini, Ulega alisema Serikali imejipanga kulipa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara na madaraja ili kuhakikisha kazi zinaendelea bila kusuasua hadi kukamilika kwa kiwango cha lami.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi, Dkt. Rhimo Nyansaho, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi wa Mara kupitia miradi ya kimkakati. Alieleza kuwa kukamilika kwa barabara hizo kutaleta mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi.
Naye Mbunge wa Serengeti, Mheshimiwa Mary Daniel Surati, aliomba barabara zote zinazounganisha wilaya ndani ya mkoa wa Mara zijengwe ili kukuza uchumi na kudumisha heshima ya Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.





