Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdalla Ulega, amesema mradi wa uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi unatekelezwa na Serikali utakuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kihistoria itakayobadilisha sura ya Jiji la Dar es Salaam na kuwa kivutio kikuu cha utalii.
Akizungumza katika hafla iliyohusisha viongozi mbalimbali wa Serikali na wadau wa maendeleo, Ulega alisema mradi huo ni sehemu ya dira ya maendeleo ya Rais Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kuboresha mazingira ya mijini, kudhibiti mafuriko na kuleta fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi.
“Mradi huu wa Bonde la Mto Msimbazi ni wa kihistoria. Utakwenda kubadilisha kabisa taswira ya Dar es Salaam na kuifanya kuwa na eneo la kisasa la burudani na utalii, jambo ambalo kwa miaka mingi lilikuwa changamoto kwa jiji letu,” alisema Ulega.
Alieleza kuwa kupitia mradi huo, maeneo ya kandokando ya mto yataboreshwa na kujengwa bustani za kisasa, maeneo ya mapumziko (recreational areas) pamoja na miundombinu rafiki kwa watalii, hatua itakayowezesha wageni na wakazi kufurahia mandhari ya jiji hilo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, utekelezaji wa mradi huo utafungua fursa ya shughuli za utalii wa ndani ya jiji, ikiwemo uwezekano wa huduma za usafiri wa majini katika mto huo, hali itakayowawezesha watu kuona vivutio mbalimbali vya Dar es Salaam kwa mtazamo tofauti.
Aidha, Ulega alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio makubwa ya Serikali katika sekta ya ujenzi wa barabara nchini, akibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupanua mtandao wa barabara ukilinganisha na ilivyokuwa wakati wa uhuru.
“Tanzania ina mtandao mkubwa wa barabara unaoendelea kukua kila mwaka. Tumejenga maelfu ya kilomita za barabara za lami na nyingine zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Hii inaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha miundombinu,” alisema.
Alisisitiza kuwa maendeleo hayo ni matokeo ya juhudi za viongozi mbalimbali waliopita, akiwemo Baba wa Taifa Julius Nyerere, Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa, Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete, na Hayati John Magufuli, huku akibainisha kuwa kasi hiyo inaendelezwa kwa nguvu chini ya uongozi wa Rais Samia.
Ulega aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali za Mitaa kuhakikisha miradi ya barabara na miundombinu inatekelezwa kwa ufanisi, huku akiwataka wataalam kushirikiana kikamilifu pale viongozi wanapofanya ziara ili kutoa majibu sahihi kwa wananchi.
Alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuwa na imani na Serikali yao, akisisitiza kuwa nchi imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa miundombinu na itaendelea kufanya hivyo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Mradi huu wa Msimbazi ni urithi (legacy project) wa Rais Samia, na utaendelea kukumbukwa kwa vizazi vingi vijavyo,” alisisitiza Ulega.






