Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea ujumbe wa ngazi ya juu kutoka Mtandao wa Viongozi Wanawake Afrika (AFLN) katika Ikulu ya Dar es Salaam, ukiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya utawala bora, ujenzi wa amani na uongozi wa wanawake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari S. Machumu, ujumbe huo ulihusisha viongozi wanawake waandamizi kutoka barani Afrika na taasisi za kimataifa, akiwemo Rais wa zamani wa Liberia, Mheshimiwa Ellen Johnson Sirleaf, pamoja na Rais wa zamani wa Ethiopia, Mheshimiwa Sahle-Work Zewde.
“Tanzania imepongezwa kwa hatua iliyopiga katika kurejesha hali ya amani na utulivu kufuatia matukio yaliyojitokeza baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, pamoja na juhudi za serikali za kulinda umoja wa kitaifa na kurejesha shughuli za kiuchumi na kijamii,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa ujumbe huo ulitambua mchango wa Tanzania kama nguzo ya amani, utulivu na maridhiano barani Afrika, huku ukisisitiza uongozi wa Rais Samia katika kuiongoza nchi kupitia kipindi kigumu kwa kudumisha uadilifu wa taasisi na utulivu wa umma.
Katika mazungumzo yao, kwa mujibu wa Bw. Machumu, ujumbe huo ulisisitiza umuhimu wa kuendeleza mageuzi ya kidemokrasia, kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ushiriki wa wananchi katika maamuzi, sambamba na kupanua fursa za uongozi kwa wanawake katika ngazi zote.
“Tumejipanga kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kulea kizazi kipya cha viongozi wanawake barani Afrika, kwa kuweka mifumo itakayowawezesha wanawake kufikia na kufanikiwa katika nafasi za uongozi,” ilieleza taarifa hiyo ikinukuu ujumbe huo.
Kwa upande wake, Rais Samia alishukuru kwa ziara hiyo na majadiliano yenye tija, akisisitiza dhamira ya serikali ya kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa kijamii, pamoja na kuendelea na mageuzi ya utawala na taasisi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Samia pia alieleza kuwa Tanzania itaendelea kupanua fursa za uongozi kwa wanawake na vijana huku ikizingatia misingi ya kidemokrasia, ushirikishwaji na maendeleo endelevu.
Aidha, alisisitiza kuwa nchi itaendelea kushirikiana na wadau katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuimarisha maendeleo na ustawi wa wananchi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mkutano huo ni sehemu ya mawasiliano endelevu kati ya serikali na washirika wa kimkakati, yakilenga kuimarisha nafasi ya Tanzania kama taifa lenye utulivu, linalotekeleza mageuzi na lenye mwelekeo wa maendeleo ya baadaye.
Mtandao wa Viongozi Wanawake Afrika (AFLN), unaoungwa mkono na African Union na United Nations, unalenga kuendeleza uongozi wa wanawake, ujenzi wa amani na utawala bora barani Afrika.




