Na.SOPHIA KINGIMALI.
Katika kipindi ambacho taifa linaendelea kurejea katika hali ya utulivu kufuatia changamoto mbalimbali zilizojitokeza nchini, waandishi wa habari wametakiwa kutumia taaluma yao kama nyenzo ya kuunganisha jamii na siyo kuigawa.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipokutana na viongozi wa klabu za waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali nchini
Msigwa amesema kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kulinda mshikamano wa kitaifa, hasa katika nyakati nyeti za kisiasa, akieleza kuwa kalamu za waandishi zina nguvu kubwa inayoweza kujenga au kubomoa jamii.
Msigwa amebainisha kuwa katika mazingira ya sasa, ni muhimu kwa wanahabari kuchagua kwa umakini taarifa wanazozitoa ili kuhamasisha amani, akionya dhidi ya matumizi mabaya ya vyombo vya habari vinavyoweza kuchochea migogoro.
Aidha, ameeleza kuwa maendeleo ya teknolojia yamepanua wigo wa usambazaji wa habari, ambapo mtu mmoja anaweza kufikia hadhira kubwa kupitia mitandao ya kijamii, hali inayoongeza wajibu wa uwajibikaji kwa kila mtoa taarifa.
Akizungumzia mwelekeo wa tasnia hiyo, Msigwa amesema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kuchochea maendeleo ya taifa, ikiwa ni pamoja na kufanikisha dira ya maendeleo ya mwaka 2050, endapo vitatumika kwa weledi na maadili.
Kwa upande mwingine, ameonya kuwa mwenendo wa baadhi ya vyombo vya habari duniani umekuwa ukichochea chuki na migogoro, hali inayopaswa kuepukwa nchini kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo.
Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwajengea uwezo waandishi wa habari kupitia mafunzo yatakayofanyika katika mikoa mbalimbali, kwa lengo la kuimarisha utendaji wao na mchango wao katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji UTPC Kenneth Simbaya amewataka waandishi nchini kuhakikisha wanazingatia weredi pindi wanapotekeleza wajibu wao.
Nae,msemaji wa jeshi la polisi kamanda David Misime amesema jeshi hilo litaendelea kushirikiana na waandishi na pindi itakapotokea changamoto watahakikisha inatatukiwa kwa wakati.





