MAENDELEO Bank PLC imeendelea kuweka rekodi ya kipekee kwa kupata faida kwa miaka 11 mfululizo tangu mwaka 2015, hali inayoonesha uimara wa biashara, uongozi wenye maono, pamoja na utekelezaji thabiti wa mikakati ya ukuaji endelevu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Aprili 14, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Fedha, Nolasco Charles, amesema kuwa benki imeendelea kuonesha mafanikio makubwa ya kifedha, yakithibitisha uwezo wake wa kuhimili ushindani wa soko.
Aidha, ameeleza muhtasari wa matokeo ya kifedha kuwa ni kama ifuatavyo:
Jumla ya mapato: TZS 29.05 bilioni, kutoka TZS 23.00 bilioni mwaka 2024 (ukuaji wa asilimia 26).
Mapato halisi yatokanayo na riba: TZS 25.78 bilioni, kutoka TZS 20.06 bilioni (ukuaji wa asilimia 28).
Faida kabla ya kodi: TZS 5.02 bilioni, kutoka TZS 3.85 bilioni (ukuaji wa asilimia 30).
Faida baada ya kodi: TZS 4.75 bilioni, kutoka TZS 3.68 bilioni (ukuaji wa asilimia 29). Uwiano wa gharama kwa mapato (CIR): asilimia 61.25.
Amesema ukuaji huu umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuimarika kwa biashara ya mikopo pamoja na kuongezeka kwa imani ya wateja.
Aidha, kitabu cha mikopo kimekua kwa asilimia 23, huku ubora wake ukiendelea kuimarika kufuatia kupungua kwa mikopo chechefu hadi asilimia 4.51 kutoka asilimia 4.76 mwaka uliotangulia.
Kwa upande wa amana za wateja, zimeongezeka kwa asilimia 31 kutoka TZS 104.02 bilioni mwaka 2024 hadi TZS 136.20 bilioni mwaka 2025, zikionesha uhusiano imara kati ya benki na soko.
Vilevile, jumla ya mali na mtaji wa benki vimeendelea kuimarika, kutoka TZS 104.02 bilioni mwaka 2024 hadi TZS 136.26 bilioni, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 30. Hali hii inaipa benki nafasi nzuri ya kupanua shughuli zake kimataifa.
Kubwa zaidi ni ukuaji wa zaidi ya asilimia 600 wa thamani ya hisa za benki katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, kutoka shilingi 38 mwezi Aprili 2025 hadi shilingi 2,480 tarehe 13 Aprili 2026, jambo linaloonesha imani kubwa ya soko kwa MAENDELEO Bank PLC.
Ameongeza kuwa mafanikio haya yamejengwa juu ya utekelezaji madhubuti wa mpango mkakati wa miaka sita (2025–2030), unaolenga kuimarisha rasilimali watu, kuendeleza mageuzi ya kiteknolojia, pamoja na kukuza biashara.
Benki imeendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya kidijitali, ikiwemo huduma za Mobile Banking na Internet Banking, hatua iliyoongeza ufanisi, kasi ya utoaji huduma, pamoja na kuboresha uzoefu wa wateja.
Aidha, benki imeweka mkazo katika usimamizi madhubuti wa vihatarishi (risk management) ili kuhakikisha ukuaji wake unaendelea kuwa imara na endelevu.
Akizungumzia mwaka 2026, amesema mkakati utaendelea kumweka mteja mbele katika kila jambo, huku benki ikijipanga kutoa suluhisho bunifu, rahisi na bora kwa wateja, pamoja na kuimarisha vyanzo vya mapato na kuweka kipaumbele katika mafanikio endelevu.
Amehitimisha kwa kutoa shukrani kwa wafanyakazi wote wa MAENDELEO Bank PLC kwa kujitolea kwao, pamoja na kuwashukuru wateja kwa kuendelea kuiamini benki.
