MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude akizungumza kwenye halfa hiyo jijini Arusha leoMeneja wa TANESCO Mkoa wa Arusha, Mhandisi Kisika Kisika akizungumza kwenye hafla hiyo jijìni Arusha

Happy Lazaro,Arusha .

Arusha.MKUU wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ametoa onyo kali kwa watumishi dhidi ya matumizi mabaya ya magari mapya yaliyokabithiwa huku akisisitiza kuwa ni mali ya umma inayopaswa kulindwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mkude ameyasema hayo Aprili 13,2026 jijini Arusha 

katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika ofisi za TANESCO mkoani hapa.

Mkude amesema kuwa serikali imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuimarisha huduma za nishati nchini baada ya kukabidhi vitendea kazi vipya kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Arusha, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kupunguza changamoto za umeme kwa wananchi.

Mkude amesema kuwa, serikali imetumia takribani shilingi bilioni 1.4 kununua magari hayo, yakiwemo yenye kreni, magari ya kiutendaji pamoja na bajaji, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za umeme mijini na vijijini.

“Rasilimali hizi zimegharimu fedha nyingi za walipa kodi, hivyo ni lazima zitumike kwa uadilifu mkubwa. Hatutavumilia matumizi yasiyo sahihi ya magari haya kwa maslahi binafsi,” alisisitiza Mkude.

Ameongeza kuwa ujio wa vitendea kazi hivyo utaiwezesha TANESCO kuongeza kasi ya kushughulikia hitilafu za umeme, kufikia maeneo ya pembezoni kwa urahisi na kuboresha huduma kwa wananchi kwa wakati.

Mkude amebainisha kuwa serikali ya awamu ya sita imeendelea kuwekeza katika ununuzi wa Vitendea kazi vya sekta hiyo ambapo kwa mwaka 2025/26, jumla ya Shilingi Bilioni 180 zilitolewa kununua vyombo vya usafiri 802 huku pia Shilingi Bilioni 200 zikitengwa kwa mwaka 2026/27 kwaajili ya ununuzi wa vyombo vingine vya usafiri kama sehemu ya kimkakati katika kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Aidha Mkude amesisitiza umuhimu wa utunzaji wa magari na vifaa vya usafiri vinavyonunuliwa na Serikali, akisema vitu hivyo vinanunuliwa kwa gharama kubwa kwaajili ya kuhudumia wananchi, hivyo ni muhimu kutunzwa na kutumika kwa ilivyodhamiriwa.

Naye Meneja wa TANESCO Mkoa wa Arusha, Mhandisi Kisika Kisika, amesema upatikanaji wa magari hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha taasisi za umma zinapata vitendea kazi vya kutosha ili kuongeza ufanisi.

Amesema kuwa Mkoa wa Arusha una hali nzuri ya upatikanaji wa umeme, ukipokea nishati kutoka vituo vitatu vikuu vya Njiro, Lemguru na Karatu, hali inayouweka mkoa huo katika nafasi nzuri ya kuvutia uwekezaji.

Hata hivyo, Kisika amebainisha kuwa matumizi ya umeme bado ni ya chini, ambapo mkoa unatumia takribani asilimia 30 tu ya umeme unannatikana huku zaidi ya asilimia 60 ikiwa ni ziada ambayo haijatumika .

Ameongeza kuwa kwa sasa mkoa una zaidi ya wateja laki tatu wa umeme, idadi inayoendelea kuongezeka kufuatia jitihada za serikali kusambaza huduma hiyo hadi vijijini na vitongoji.

Aidha, amesema karibu vijiji vyote mkoani humo tayari vimefikiwa na huduma ya umeme, huku hatua zikichukuliwa kuhakikisha vitongoji vyote vinaunganishwa ili wananchi wengi zaidi wanufaike na nishati hiyo muhimu.

Uongozi wa TANESCO Mkoa wa Arusha uliahidi kuyatunza. uyatumia ipasavyo magari hayo ili kuhakikisha yanaleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma kwa wateja wake .