Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, akizungumza na washiriki wa Miss World Tanzania kuhusu umuhimu wa kutumia Kiswahili kama nyenzo ya kuitangaza Tanzania kimataifa, pamoja na kuhimiza mshikamano, maadili na kulinda heshima ya taifa, Aprili 13, 2026 jijini Dodoma.
Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amesema kuwa mashindano ya urembo nchini ni jukwaa muhimu la kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili kimataifa, licha ya washiriki kulazimika kutumia lugha nyingine wanapowasiliana nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 13, 2026 jijini Dodoma kuhusu washiriki wa Miss World Tanzania, Makonda amesisitiza kuwa washiriki wanapaswa kujivunia Kiswahili kama sehemu ya utambulisho wao wanapoiwakilisha Tanzania kimataifa.
Amesema kuwa urembo ni asili ya Mungu na kila binadamu ameumbwa kwa upekee wake, hivyo mashindano hayo si ya kuangalia nani ni mrembo zaidi pekee bali ni fursa ya kutafakari ukuu wa Mungu katika uumbaji wake.
Aidha, amebainisha kuwa mashindano mbalimbali kama Miss World Tanzania na Miss Universe yanachochea ushindani chanya unaosaidia kuongeza ubora wa mashindano hayo pamoja na thamani ya zawadi, hali inayowahamasisha washiriki kujituma zaidi.
Ameongeza kuwa mshindi atakayepatikana Aprili 19 atapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania nchini Vietnam kama balozi wa taifa, hivyo anapaswa kulinda heshima ya nchi na kuepuka migawanyiko ya kikanda kwa kuwa anawakilisha Tanzania nzima.
Mhe. Makonda amesema kuwa taifa linaweza kuharibika kupitia sekta za utamaduni, michezo na habari, hivyo washiriki wanapaswa kuwa makini wanapopewa jukumu la kupeperusha bendera ya taifa.
Pia amewataka walimbwende kutambua kuwa urembo wao una kusudi, wasikubali kupoteza ndoto zao, waheshimu wazazi wao na kumtukuza Mungu katika maisha yao.
Ameeleza kuwa Tanzania imekuwa ikishiriki mashindano ya urembo kimataifa tangu mwaka 1967 kupitia mshiriki wa kwanza aitwaye Tereza, na hadi sasa nchi imepata nafasi ya kushiriki mara 29, huku wakitarajia kumpata mwakilishi wa 30 mwaka huu.
Kuhusu maandalizi ya AFCON, amesema kuwa Tanzania ipo tayari na hakuna mpango wa kuahirisha mashindano hayo, akibainisha kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha za kutosha kwa ajili ya miundombinu ya michezo na maandalizi yanaendelea vizuri, huku Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likiridhia hatua zilizofikiwa.
Kwa upande wake Muandaaji wa Shindano hilo,Mustapha Hassanali, amebainisha kuwa Mshindi wa Miss World Tanzania atapatiwa zawadi ya Shilingi Mil.10, gari pamoja na mshahara wa Mil.2 kila mwezi mpaka siku ambayo atakabidhi taji kwa Mshindi mwingine 2027.

