Na John Bukuku, Dar es Salaam
* Hali inazidi kuwa mbaya
* Yashauriwa kuacha uvutaji wa Sigara
Katika uwanja wa sera na afya ya umma, udhibiti wa matumizi ya tumbaku nchini unaweza kufananishwa na dabi kali ya soka inayohitaji umakini mkubwa, mbinu na maamuzi ya haraka.
Katika mchezo huu, uchumi unashambulia upande mmoja huku afya ya jamii ikijilinda upande mwingine—na katikati ya uwanja yupo mwamuzi mkuu wa soka hiyo ambaye ni Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Nafasi ya TMDA katika mchezo huu mgumu, inapaswa kucheza kwa tahadhari kubwa ili kuhakikisha afya ya umma inalindwa bila kuathiri kwa kiasi fulani sekta ya uchumi inayotegemea tumbaku.
“Ni kama kucheza mechi ya fainali ambapo kila uamuzi una athari kubwa. TMDA inapaswa kuhakikisha bidhaa zote zinakidhi viwango, lakini pia kuzingatia muktadha wa kiuchumi wa nchi. 
Katika kuhakikisha ushindi wa afya ya umma, Dkt.Yona H. Mwalwisi Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo anasema TMDA imeweka mifumo madhubuti ya kudhibiti ubora wa bidhaa za tumbaku pamoja na zile mbadala zenye nikotini. Hii ni sawa na kuweka safu imara ya ulinzi ili kuzuia madhara yasivuke mipaka.
Aidha, anabainisha kuwa mamlaka hiyo hushirikiana na taasisi nyingine za serikali kuhakikisha sheria zinazingatiwa, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku matangazo yanayoweza kupotosha umma kuhusu usalama wa bidhaa za tumbaku. Huu ni mkakati muhimu wa kunusuru jamii katika utumiaji wa tumbaku.
Anabainisha kuwa TMDA hushiriki katika kampeni za uelimishaji kwa umma, ikiwahamasisha wananchi kuelewa madhara ya uvutaji sigara. Hapa, elimu inakuwa silaha muhimu ya kuzuia magoli ya hatari dhidi ya afya za wananchi.
Dkt. Mwalwisi anasisitiza kuwa uelimishaji ni sehemu muhimu ya mkakati wa muda mrefu.
“Tukiwaelimisha wananchi, tunawapa uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao,” anabainisha.
“Hata hivyo, changamoto bado ni nyingi. Uwepo wa bidhaa bandia au zisizokidhi viwango, ” anasema Mwalwisi
Hii ni kama uchezaji wa hatari uwanjani unaoweza kusababisha madhara miongoni mwa wachezaji, na kuongeza hatari kwa uànuzi wa refari uwanjani ama watumiaji wa bidhaa hizo.
TMDA imeendelea kuimarisha ukaguzi wa bidhaa zinazoingia nchini ili kuhakikisha hazisambazwi bila kuthibitishwa ubora wake. Hatua hii ni sawa na kuongeza ulinzi mkali langoni ili kuzuia magoli yasiyo halali.
Lakini kwa upande mmoja, tumbaku ni zao la kimkakati linaloingizia taifa fedha za kigeni na kuinua maisha ya wakulima.
Takwimu zinaonesha kuwa mapato ya sekta hiyo yaliongezeka kutoka dola milioni 897.1 mwaka 2023/2024 hadi dola milioni 1,164.3 mwaka 2024/2025, huku mauzo ya nje yakifikia zaidi ya dola milioni 516.9.
Anaeleza mafanikio hayo, Stanley Nelson Mnozya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku,
“Zao la tumbaku lina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, hasa katika kuongeza fedha za kigeni na kipato cha wakulima.” anasema Stanley.
Tausi Juma mkulima wa Tumbaku na mkazi wa Ibushi Tabora anaeleza kuwa uzoefu alioupata tangu utotoni umemjengea nidhamu na uelewa mpana wa mnyororo mzima wa zao la tumbaku, kuanzia maandalizi ya shamba hadi uuzaji.
Anasema kwa sasa anashirikiana kwa karibu na wataalamu wa kilimo wanaompa ushauri wa kitaalamu kuhusu mbegu bora, matumizi sahihi ya pembejeo na udhibiti wa magonjwa ya mimea, jambo linalomsaidia kuongeza tija na ubora wa mazao yake kila msimu. Aidha, ameweza kuwahamasisha wakulima wenzake kijijini kwake kuzingatia kilimo chenye tija kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji.
Pia Tausi anabainisha kuwa mafanikio yake yamemuwezesha kuboresha maisha ya familia yake na jamii inayomzunguka, ikiwemo kutoa ajira za msimu kwa vijana wakati wa kupanda, kuvuna na kuchakata tumbaku.
Anasema ana ndoto ya kupanua zaidi shughuli zake kwa kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kilimo na uhifadhi ili kuongeza thamani ya zao hilo. Kupitia juhudi zake, Tausi anaamini tumbaku itaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa familia yake na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake Mratibu wa Kinga ya Magonjwa Yasiyoambukiza na Udhibiti wa Matumizi ya Tumbaku kutoka Wizara ya Afya Tanzania, Goodluck Tumaini anarejelea madhara yaliyoelezwa na TMDA kuhusu utumiaji wa tumbaku akisema kuwa matumizi ya tumbaku yana athari kubwa kwa afya ya binadamu ikiwa ni pamoja na kusababisha magonjwa kama saratani, shinikizo la juu la damu, kisukari na magonjwa sugu ya mapafu.
Anasema kuwa saratani ya mapafu ni miongoni mwa magonjwa makubwa yanayohusishwa moja kwa moja na matumizi ya tumbaku, kutokana na athari zake katika mfumo wa upumuaji.
Lakini kwa upande wa utabibu Daktari bingwa wa saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dkt. Emmanuel Lugina, anasema moshi wa tumbaku una zaidi ya kemikali 7,500, ambapo kati ya hizo zaidi ya 250 zina madhara kwa binadamu na takriban 70 zimethibitishwa kusababisha saratani ya mapafu.
Dkt. Lugina amesema kemikali hizo zimegawanyika katika makundi makuu matatu ambayo ni Tobacco-specific nitrosamines (TSNAs) kama NNK, Polycyclic aromatic hydrocarbons (PAHs) kama benzopyrene, pamoja na kemikali nyingine hatarishi zikiwemo benzene, formaldehyde na metali nzito kama arsenic, cadmium na chromium.
Anaongeza kuwa moshi huo pia una free radicals zinazochochea uharibifu wa seli kupitia oxidative stress.
Amefafanua kuwa kemikali hizo huathiri seli za mapafu kwa hatua kadhaa za kitabibu, ambapo kwanza husababisha uharibifu wa DNA kwa kutengeneza DNA adducts, hali inayosababisha makosa wakati seli zinapojigawa.
Aidha, mabadiliko hayo husababisha hitilafu kwenye vinasaba muhimu kama p53, hali inayochochea ukuaji holela wa seli ambao ndio chanzo cha saratani.
Akizungumzia tofauti ya hatari, Dkt. Lugina anasema uvutaji wa sigara ndio sababu kuu ya saratani ya mapafu duniani, ukihusishwa na asilimia 80 hadi 90 ya vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Hali hii inaifanya dabi hii kuwa ngumu zaidi, kwani kila hatua ya kiuchumi ina athari kwa maisha ya watu.
Kuhusu muda wa hatari, amesema hakuna kiwango salama cha uvutaji, kwani hatari hutegemea muda na kiasi cha sigara kinachovutwa (pack-years).
Anaeleza kuwa hatari huongezeka zaidi baada ya miaka 20 ya uvutaji, lakini hata uvutaji wa muda mfupi una athari.
Amesisitiza kuwa kuacha kuvuta sigara kuna faida kubwa kiafya, akibainisha kuwa baada ya miaka 10 hadi 15 ya kuacha, hatari ya saratani ya mapafu hupungua kwa nusu.
Aidha, kuacha kabla ya umri wa miaka 40 kunaweza kuondoa hadi asilimia 80 hadi 91 ya hatari ya ziada.
Dkt. Lugina ameonya kuwa saratani ya mapafu mara nyingi haioneshi dalili katika hatua za awali, jambo linalosababisha wengi kugundulika wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa.
Hata hivyo, ametaja dalili muhimu zinazopaswa kufuatiliwa kuwa ni pamoja na kikohozi kisichoisha, kukohoa damu, maumivu ya kifua, kupumua kwa shida, sauti kukwaruza, kupungua uzito bila sababu na uchovu wa muda mrefu.
Ameshauri kuwa bado hali inaendelea kuwa mbaya hivyo ni muhimu wananchi kufika hospitali mapema wanapoona dalili hizo, akisisitiza kuwa mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 40 mwenye historia ya uvutaji sigara anapaswa kufanyiwa uchunguzi wa haraka ikiwemo kipimo cha X-ray au CT scan ya kifua.
“Usisubiri dalili ziwe kali. Uchunguzi wa mapema unaweza kuokoa maisha,” amesisitiza.
Amehitimisha kwa kushauri kuwa kuacha kuvuta sigara ni njia kuu ya kujikinga na saratani ya mapafu, akihimiza watu wanaovuta kupanga kuacha mara moja kwani faida zake huanza kuonekana hata baada ya muda mfupi.
