Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi (Doctor of Letters – Honoris Causa) ya Chuo Kikuu cha Jimbo la Nasarawa cha nchini Nigeria.

Rais Dkt. Samia ametunukiwa Shahada hiyo katika Sherehe ya Mahafali ya Nane ya chuo hicho iliyofanyika katika kampasi kuu ya Keffi, nchini humo, ambapo alishiriki kwa njia ya mtandao akiwa Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma.

Chuo hicho kimemtunuku Shahada hiyo Rais Dkt. Samia kwa kutambua uongozi wake wa mageuzi unaozingatia uwazi na uwajibikaji, pamoja na mchango wake katika kuimarisha uchumi wa Tanzania, kukuza ushirikiano wa kimataifa, sambamba na juhudi zake za kuimarisha nafasi ya wanawake, kusimamia afya ya mama na mtoto, kuwezesha wanawake na vijana kiuchumi kupitia Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika.

Chuo Kikuu hicho kimemtaja Rais Dkt. Samia kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya kigeni nje ya Nigeria kutunukiwa Shahada ya Heshima na chuo hicho, na miongoni mwa viongozi wanawake wachache barani Afrika waliowahi kushika nafasi za juu za uongozi wa kitaifa.

Akizungumza baada ya kutunukiwa, Rais Dkt. Samia amesema amepokea heshima hiyo kwa unyenyekevu, akieleza kuwa mafanikio hayo yanaakisi juhudi za pamoja za Watanzania katika kuendeleza maendeleo na ushirikiano wa Bara la Afrika.

“Napokea heshima hii kwa unyenyekevu mkubwa. Tuzo hii si yangu pekee, bali inaakisi jitihada za pamoja za wananchi wa Tanzania katika kuendeleza maendeleo, ushirikiano na ustawi wa Bara la Afrika,” amesema Rais Dkt. Samia.

Akirejea safari yake ya uongozi, Rais Dkt. Samia amesema uzoefu wake hadi kufikia nafasi ya juu ya uongozi wa kitaifa, unatoa chachu ya kuendelea kufungua fursa na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika uongozi na maamuzi ya maendeleo barani Afrika.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuanza mazungumzo ya ushirikiano wa kitaaluma na chuo hicho ikiwemo kubadilishana wanafunzi, tafiti na programu za pamoja kwa lengo la kuimarisha mahusiano ya elimu ya juu pamoja na kuchochea maendeleo ya sayansi, utafiti na ubunifu kati ya Tanzania na Nigeria.

Chuo Kikuu cha Jimbo la Nasarawa, Keffi, ni miongoni mwa vyuo vikuu bora vya nchini Nigeria, kikishika nafasi ya pili kwa vyuo vikuu vya majimbo nchini humo, nafasi ya nane kati ya vyuo vikuu 309 vya nchini Nigeria, na nafasi ya 36 kwa vyuo vikuu vya nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Watu wengine mashuhuri waliowahi kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari na chuo hicho ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bi. Amina Mohammed, pamoja na mfanyabiashara mashuhuri barani Afrika, Bw. Aliko Dangote.