Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ferdinand Mdoe,akizungumzia ubovu wa barabara ya Songea-Namtumbo-Tunduru ambayo kwa sasa inalalamikiwa na madereva na watumiaji wengine kutokana na kuwa na mashimo mengi hali inayosababisha kutumia muda mwingi na kuharibika kwa magari(Picha na Muhidin Amri)
………..
Na Mwandishi Wetu, Tunduru
MADEREVA wa magari wanaotumia barabara ya Songea-Namtumbo-Tunduru kuelekea mikoa mingine ya Lindi-Mtwara na Dar es Slaam wamelalamikia ubovu wa barabara hiyo unoasababisha uharifu mkubwa wa vipuri vya magari ikiwemo springi na kuchanika kwa magurudumu mara kwa mara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya madereva hao wanaonza safari kati ya Songea mjini kuelekea mkoa jirani wa mtwara wamesema,barabara hiyo kwa sasa ni changamoto kubwa kwenye shughuli zao za usafirishaji kutokana na kuwa na mashimo mengi na makubwa.
Abdala Said alisema,changamoto ya ubovu wa barabara inawafanya washindwe kukamilisha fedha za wamiliki wa magari kutokana na kutumia fedha zinazopatikana kununua vipuri vya magari kama matairi ambayo yamekuwa yanaharibika mara kwa mara kutokana na ubovu wa barabara hususani mashimo makubwa yaliyopo.
Alisema,baadhi ya matajiri ambao ni wamiliki wa magari lakini hawafahamu changamoto hiyo na inapotokea hitilafu ya vyombo vyao iliyosababishwa na ubovu wa barabara,wamekuwa wakiwanyang,anya magari kwa madai kuwa wazembe na wameshindwa kuyatunza.
“baadhi ya wamiliki wa magari ambao wako hapa Ruvuma na wengine wanaishi nje wanajifanya hawajui kabisa changamoto ya barabara hii,ukimweleza mmiliki kwamba gari imeharibika au kuanguka anakwambia haufai na kukataa kukupa posho yako ya safari na kama derena huna mkataba kinachofuatia ni kunyang,anywa gari”alisema.
Dereva mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Ndunguru anayeendesha basi linalofanya safari zake kati ya Songea na Tunduru Mkoani Ruvuma,amelalamikia kuwepo kwa mashimo makubwa katikati ya barabara ambayo kwa muda mrefu sasa hayajafukiwa hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa magari na hata kupinduka.
Ndunguru,ameiomba Serikali kupitia wakala wa barabara Tanzania(TANROADS)Mkoa wa Ruvuma kuchukua hatua ya haraka kufanya matengenezo ya barabara hiyo kwa manufaa ya wamiliki,madereva na wasafiri ambao kwa sasa wanatumia muda mrefu kusafiri kati ya Songea na Tunduru.
“Awali tulikuwa tunatumia masaa 3.30 hadi 4 kutoka Songea hadi Tunduru lakini kutokana na changamoto hiyo hususani uwepo wa mashimo mengi tunatumia masaa 5 hadi 6,tunaomba sana vyombo vya Habari mtufikishie kilio chetu kwa serikali juu ya ubovu wa barabara hii”alisema Ndunguru.
Baadhi ya abiria wanaotumia barabara hiyo kusafiri kutoka Songea kuelekea mikoa jirani ya Lindi na Mtwara,wameeleza namna ubovu wa barabara unavyowaathiri hasa wanapopata dharura kwa kutakiwa kusafiri.
Frank Lambeli alisema,kutokana na changamoto hiyo hata idadi ya mabasi kwa kiasi kikubwa yamepungua na kutolea mfano mabasi ya kampuni ya Baraka ambayo yalikuwa yanatoa huduma ya usafiri kati ya Mkoa wa Ruvuma,Lindi na Dar es slaam kusitisha safari zake.
“Hii barabara kwa sasa ni janga kubwa sana,yaani ina mashimo mengi yanayosababisha magari kutembea pole pole tunashindwa kufika tunakokwenda kwa muda sahihi,tunawaomba watu wa Tanroads kuifanyia kazi badala ya kutumia muda mwingi kukaa ofisini”alisema Lambeli.
Kwa upande wake kaimu meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Ferdinand Mdoe,amekiri uwepo kwa changamoto ya mashimo kwenye barabara hiyo ambao yanazaliwa kila siku na ya zamani yanazidi kuongezeka ukubwa.
“uwa tunafanya jitihada ya kukarabati sehemu korofi zenye mashimo lakini uwa kunajitokeza mashimo mapya,lakini katika barabara ya Songea-Namtumbo hadi Tunduru kwa mwaka huu tuna miradi takribani minne ili kukabiliana na hali hiyo na katika ukaguzi wetu wa mwisho tumebainisha maeneo yanayotakiwa kufanyiwa kazi”alisema Mdoe.




