Na Heri Shaaban, Dar es Salaam

TAASISI ya Fahari Tuamke Maendeleo imeadhimisha Siku ya Matendo Mema Duniani kwa kupanda miti na kuchangia damu katika Zahanati ya Mvuti iliyopo Kata ya Msongola, jijini Dar es Salaam.

Madhimisho hayo yalifanyika katika Zahanati ya Mvuti, Wilaya ya Ilala, ambapo wanachama wa taasisi hiyo walipanda miti, walijitolea damu, walifanya usafi wa mazingira pamoja na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo, Neema Mchau, alisema kuwa taasisi hiyo ina jukumu la kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matendo mema katika jamii.

Alieleza kuwa pamoja na kuwahamasisha watu kutenda mema, taasisi imekuwa ikitoa elimu ya mazingira shuleni kwa kushirikiana na wanafunzi kupanda miti, pamoja na kupanda miti hospitalini na kuchangia damu.

Aliongeza kuwa hatua ya kuchangia damu ni muhimu kutokana na ongezeko la ajali zinazotokea kila siku, hali inayosababisha uhitaji mkubwa wa damu katika hospitali za serikali.

“Kila mwaka taasisi yetu hushiriki maadhimisho ya Siku ya Matendo Mema Duniani kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwa ni pamoja na kutembelea makundi maalum. Mwaka huu tumeshiriki kupanda miti katika Shule ya Kiboga, Shule ya Mvuti, Gunatra Secondary pamoja na Zahanati ya Mvuti, na tumefanikiwa kuchangia chupa 12 za damu,” alisema Neema.

Aidha, alibainisha kuwa huu ni mwaka wa tano kwa taasisi hiyo kushiriki maadhimisho hayo, ambapo hapo awali waliadhimisha katika Wilaya ya Kisarawe na Ilala, maeneo ya Yongwe na Chanika.

Alitoa wito kwa jamii kuendeleza utamaduni wa kutenda mema katika familia na jamii kwa ujumla ili kuwajenga vijana kuwa na maadili mema na kuepuka kujiingiza katika makundi yasiyofaa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkera, Kata ya Msongola, Waziri Moshi Singilimo, aliipongeza Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo kwa juhudi zao za kuadhimisha siku hiyo kwa vitendo, ikiwemo kupanda miti 100 katika eneo la Zahanati ya Mvuti.

Naye Muuguzi Mfawidhi wa Zahanati ya Mvuti, Paulina Ngoso, aliipongeza taasisi hiyo kwa mchango wake katika kuboresha mazingira na huduma za afya kupitia usafi na upandaji miti, na kutoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono juhudi hizo.