Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omari, amesema kuwa serikali itaendelea kuimarisha sekta ya fedha ili iwe chachu ya maendeleo ya haraka ya kiuchumi nchini.
Amesema hayo leoApril 9,2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua jukwaa la wadau wa sekta ya fedha la mwaka 2026 lenye kauli mbiu isemayo “Sekta ya fedha bunifu na yenye uwajibikaji kwa maendeleo endelevu na jumuishi ya jamii na uchumi”.
Katika hotuba yake, Waziri Omari ameeleza kuwa jukwaa hilo lina lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya fedha ili kujadili utekelezaji wa mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha wa miaka kumi (2021–2029) huku akisisitiza kuwa sekta hiyo ina nafasi muhimu katika kukuza uchumi na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi.
“Sekta ya fedha ni mhimili muhimu wa maendeleo ya taifa. Tunahitaji kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi wote kwa urahisi na kwa gharama nafuu,” amesema Waziri Omari.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba, amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za fedha, ongezeko la matawi na mawakala wa benki, pamoja na ukuaji wa huduma za fedha kwa njia ya kidijitali.
Amebainisha kuwa asilimia 76 ya Watanzania sasa wanapata huduma rasmi za kifedha, hatua inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya simu za mkononi na huduma za fedha mtandao.
Naye, Naibu waziri wizara ya fedha Mhandisi Mshamu Munde ameeleza umuhimu wa kuendelea kudhibiti hatari za kifedha ikiwa ni pamoja na biashara haramu na matumizi mabaya ya mifumo ya fedha, huku akisisitiza usimamizi madhubuti wa teknolojia mpya za kifedha.
Aidha Washiriki walipata fursa ya kujadili changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya fedha, hususan katika maeneo ya ubunifu wa teknolojia, ujumuishwaji wa kifedha na uwekezaji.
Akihitimisha hotuba yake, Waziri Omari amewataka wadau kutumia jukwaa hilo kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha sera, sheria na mifumo ya kifedha ili kufikia lengo la kuwa na uchumi imara unaotegemea sekta ya fedha ifikapo mwaka 2050.
Jukwaa hilo linatarajiwa kutoa maazimio yatakayosaidia kuimarisha sekta ya fedha na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Pia,Jukwaa hilo pia lilihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa mabenki, taasisi za bima, vyama vya ushirika, pamoja na sekta binafsi.





