Serikali imesema itaijenga barabara ya Kakonko kwenda mpaka wa Muhanga kupitia Gwarama (km 41.43) kwa kiwango cha lami ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi na wafanyabiashara.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya leo, Aprili 8, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kakonko Mhe. Alan Thomas Mvano, lililouliza Je, lini barabara ya Kakonko kwenda mpaka wa Muhange kupitia Gwarama (km 41.43) itajengwa kwa kiwango cha lami.
Eng. Kasekenya amesema kuwa barabara hiyo ni barabara Kuu inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma ambapo kwa sasa Serikali ipo katika hatua ya kutafuta fedha ili kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni ni hatua ya awali katika mchakato wa kuijenga kwa kiwango cha lami.
Aidha, Naibu Waziri Kasekenya ameongeza kuwa Usanifu utakapokamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma kuhakikisha anaikagua na kuifanyia ukarabati barabara hiyo ili iweze kupitika na wananchi kuweza kupata huduma bora za usafiri na usafirishaji wakati ikisubiri kuengwa kwa kiwango cha lami.
