Na Imani Mtumwa Maelezo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa amesema viongozi wamepigania nchi ili kuona vizazi vinavyokuja vinaweza kujiongoza na kujitawala bila ya ubaguzi na kuendelea kunufaika na maendeleo waliyoyapigania.
Ameyasema hayo katika ziara ya kusoma dua katika Kaburi la Marehemu Hamid Ameir Ali Donge Wilaya ya Kaskazini B Unguja amesema Wazee hao wameacha alama ambayo inaendelea kukumbukwa na vizazi vilivyopo na vijavyo.
Amesema kuwa waasisi hao wamehakikisha vizazi vijavyo vinakuwa na mwelekeo mzuri wa kujitawala na kuleta maendeleo kwa kuipambania nchi ili iwe katika hali ya usalama, amani, utulivu, upendo na mshikamano ili kuiunganisha jamii kwa pamoja.
“Hii ni sababu inayopelekea kuona imani, utu na ubinaadamu wao walionao wazee wetu kwa maslahi ya watu wao waishi wakiwa na furaha na amani” ameeleza Mhe. Kitwana.
Amefahamisha kuwa Serikali inaendelea kuthamini michango wa waasisi na viongozi wa Mapinduzi hivyo jamii inawajibu wa kuimarisha mashirikiano na jitihada za viongozi hao pamoja na kuilinda nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu.
Ameeleza kuwa ni wajibu wa wananchi wote kuthamini mafanikio yaliyopatikana katika nchi kupitia waasisi hao ili iweze kutambuliwa na vizazi vijavyo pamoja na kuwaombea dua ili iwe sadaka kwao.
Kwa upende wake mtoto wa Marehemu Hamid Ameir Ali Ndugu Sarhan Hamid Ameir ameishukuru Serikali kwa kuendeleza jitihada za kuwakumbuka wazeee hao pamoja na kuiomba Serikali kuongeza jitihada katika historia ya Wazee hao ili waweze kutambuliwa na jamii jinsi walivyoitumikia nchi.
Maadhimisho ya wiki ya kuwaenzi viongozi wa Kitaifa, Waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Katibu wa kwanza wa Chama cha Afro Shirazi huadhimishwa kila ifikapo April, 7 ya kila mwaka.

