NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Baada ya kutoka sare tatu mfululizo, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga imeibuka na ushindi wa mabao 3-0, dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons, katika mechi iliyopigwa Kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, jijini, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, Allan Okello, aliyejiunga na Yanga dirisha dogo la Januari 2026, akitokea Vipers SC ya kwao Uganda, alifunga bao la kwanza kwa kichwa dakika ya 50, akipokea pasi ya Israel Mwenda, likiwa ni la pili kwake kwa msimu huu.
Wakati maafande wa Prisons wakipambana kusawazisha, walijikuta wakifungwa bao lingine la pili dakika ya 68, lililofungwa na kiungo wa timu hiyo, Mudathir Yahya, aliyeunganisha mpira uliopigwa na nyota wezake kikosini humo, Allan Okello.
Jahazi la maafande wa Prisons, lilijikuta likizidi kuzama, baada ya kiungo, Pacome Zouzoua, kuiandikia Yanga bao la tatu dakika ya 86, akimalizia mpira mrefu uliopigwa kwa ustadi wa hali ya juu na Duke Abuya na kumshinda kipa, Mussa Mbisa.
Ushindi kwa Yanga umeifanya timu hiyo kurejesha matumaini ya kutetea taji hilo, baada ya kutoka sare mechi zake tatu mfululizo, ikianza na suluhu (0-0), dhidi ya Azam FC na TRA United, kisha pia bao 1-1, mbele ya kikosi cha Mtibwa Sugar.
Kiujumla kwa msimu huu, Yanga imecheza mechi 17 za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo imeshinda 12 na kutoka sare tano, ikiendelea kujikita kileleni mwa msimamo na pointi 41, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 35 na kuruhusu matatu.
Prisons iliyoanza msimu huu na Kocha, Mkenya Zedekiah ‘Zico’ Otieno, aliyeondoka Februari 25, 2026, imecheza mechi 18 za Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo kati ya hizo imeshinda tatu, sare nne na kupoteza 11, ikiwa nafasi ya 15 na pointi 13.
Otieno aliyejiunga na Prisons, Julai 24, 2025, kwa msimu wa 2025-2026, aliiongoza timu hiyo ya maafande katika mechi 14, za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo alishinda tatu tu, sare tatu na kupoteza nane, ikifunga mabao nane na kuruhusu 16.
Katika mechi hizo 14, Otieno aliiacha Prisons ikiwa nafasi ya 14 na pointi zake 12, huku Mkenya huyo akizifundisha pia, Gor Mahia FC, Sony Sugar, Posta Rangers na KCB FC zote za kwao Kenya na timu ya taifa ya Kenya maarufu ‘Harambee Stars’.
Kwa upande wa Nsajigwa aliyejiunga na timu hiyo Februari 27, 2026, akitokea Transit Camp inayoshiriki Championship msimu huu, ameiongoza Prisons katika mechi nne, akiwa hajapata ushindi wowote, baada ya kuchapwa mitatu na kutoka sare mmoja.
