Kwa hisani ya Daily Nation
Maafisa wanne wa uhasibu kutoka Wizara ya Nishati, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) pamoja na Kampuni ya Bomba la Mafuta Kenya (Kenya Pipeline Company) wanachunguzwa kwa tuhuma za kusaidia kusababisha uhaba wa mafuta nchini pamoja na uchakachuaji wa mafuta.
Katibu Mkuu wa Nishati anayeshughulikia Petroli, Mohammed Liban na mfanyakazi wake Joseph Wafula, Mkurugenzi Mkuu wa EPRA Daniel Kiptoo pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kenya Pipeline Joe Sang walikamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Walizuiliwa katika vituo tofauti vya polisi kabla ya kuhamishiwa makao makuu ya DCI yaliyopo barabara ya Kiambu Ijumaa mchana. Maafisa zaidi wanatafutwa na DCI kama sehemu ya uchunguzi mpana kuhusu tuhuma za kuingilia mnyororo wa usambazaji wa mafuta ya petroli.
Katika operesheni ambayo vyanzo vinasema ilianza Alhamisi usiku, washukiwa walikamatwa majumbani mwao ambako kiasi kisichobainishwa cha fedha pamoja na nyaraka mbalimbali kilipatikana kusaidia uchunguzi.
Vyanzo mbalimbali vya polisi vimesema kuwa watu hao wanne wanakabiliwa na mashtaka chini ya Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi, hususan yanayohusiana na kushindwa kuweka kumbukumbu sahihi za mafuta, akiba na hifadhi ya bidhaa za petroli. Inadaiwa kuwa kushikiliwa kwa mzigo huo wa mafuta kulisababisha kuvurugika kwa usambazaji na kuzua uhaba, hali iliyohusishwa kimakosa na mgogoro wa Iran.
Mamlaka pia zinachunguza madai kuwa mzigo wa mafuta uliokuwa chini ya makubaliano ya serikali kwa serikali (G-to-G) ulipingwa kutokana na wasiwasi wa ubora, jambo lililozua hofu ya kuvurugika kwa upatikanaji wa mafuta nchini.
