*Wadau wavutiwa na fursa West Kilimanjaro, TFS yawasaka wawekezaji mahiri

Na Mwandishi Wetu, Siha

Fursa mpya ya kiuchumi kupitia uvunaji wa utomvu imeibuka na kuanza kuvutia wadau wa sekta ya misitu kufuatia mawasilisho na maonesho ya vitendo yaliyofanyika katika Shamba la Miti la West Kilimanjaro, Wilaya ya Siha, Kilimanjaro yakilenga kuongeza thamani ya rasilimali za misitu bila uharibifu.

Tukio hilo lililoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na sekta binafsi leo Aprili 3,2026, lilijumuisha mafunzo ya kitaalamu, uzoefu wa wadau pamoja na usaili wa kampuni zinazoweza kuwekeza katika shughuli za uvunaji wa utomvu.

Akifungua rasmi programu hiyo, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Mkurugenzi wa Menejimenti na Matumizi ya Rasilimali Misitu, (DCC) Salehe Beleko alisema TFS imejipanga kugeuza sekta ya misitu kuwa chanzo kikubwa cha mapato kupitia matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo.

Alisema zao la utomvu lina uwezo mkubwa wa kuongeza mapato ya taasisi na wakati huo huo kufungua ajira kwa wananchi wanaoishi jirani na misitu.

“Tunatafuta njia mbadala za kuongeza thamani ya misitu bila kuikata. Utomvu ni jibu mojawapo,” alisisitiza DCC Beleko.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mhifadhi Mkuu wa West Kilimanjaro Forest Plantation, PCO Robert Faida, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa TFS wa kuhamasisha uwekezaji katika bidhaa zisizo za mbao.

Katika wasilisho lake, alieleza kuwa uvunaji wa utomvu unaongeza thamani ya miti huku ukiendelea kuhifadhi uoto wa asili, hivyo kuwa suluhisho endelevu kwa maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi kwa wakati mmoja.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu kutoka Shamba la Miti la Meru–USA, SCO Ernest Madata, aliwasilisha uzoefu wa utekelezaji wa shughuli hizo na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni bora za uvunaji ili kuepusha madhara kwa miti na mazingira.

Sekta binafsi nayo haikubaki nyuma, ambapo wawekezaji kutoka kampuni ya Tanya Investment waliwasilisha teknolojia wanazotumia pamoja na masoko ya utomvu ndani na nje ya nchi, wakionesha namna zao hilo linavyoweza kuwa bidhaa ya kimkakati kibiashara.

Sambamba na hilo, TFS ilifanya usaili maalumu kwa kampuni inayojihusisha na uvunaji wa utomvu, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kupata mwekezaji mwenye uwezo wa kitaalamu.

Akizungumza wakati wa usaili huo, DCC Beleko alisema taasisi hiyo inalenga kupata mshirika atakayesaidia kuongeza tija, mapato na ajira kupitia zao hilo linalochipukia kwa kasi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni iliyoshiriki usaili huo, Ms Anna Exaud Rusibamayila, aliahidi kushirikiana kikamilifu na Serikali kwa kuzingatia miongozo yote, akieleza utayari wa kampuni yake kuwekeza katika shughuli za uvunaji utomvu nchini.

Tukio hilo lilihitimishwa kwa maonesho ya vitendo ya uvunaji wa utomvu msituni, hatua iliyowapa washiriki uelewa wa moja kwa moja wa shughuli hiyo na kuchochea hamasa ya kuichangamkia fursa hiyo mpya ya kiuchumi.