image.png
Na Elimu ya Afya kwa Umma.
Naibu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Shemsa Said, amesema kuwa Mafunzo kwa viongozi wasimamizi wa huduma za chanjo (Mid-level Managers Training in Immunization Services – MLM) yanalenga kuimarisha ushirikishwaji wa viongozi katika ngazi zote ili kuhakikisha huduma za chanjo zinatolewa kwa ufanisi na ubora unaotarajiwa nchini.

Dkt. Shemsa ameyasema hayo jijini Arusha wakati wa mafunzo hayo yanayowakutanisha wataalam wa afya kutoka mikoa mbalimbali, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa afya ni msingi muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mipango ya chanjo. Amesema kuwa kupitia mafunzo hayo, viongozi wanajengewa uwezo wa kupanga, kusimamia na kufuatilia huduma za chanjo kwa ufanisi zaidi katika maeneo yao.

“Mafunzo ya MLM yanaenda kuimarisha ushirikishaji na kuweza kuleta ufanisi huduma za chanjo katika jamii na kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo”amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Tumaini Haonga, amesema kuwa mafunzo hayo yamehusisha Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara pamoja na Halmashauri 184 ambapo washiriki waligawanywa katika Kanda sita (6) ili kuhakikisha ufanisi wa utoaji wa mafunzo.

Dkt. Haonga ameeleza kuwa lengo kubwa la mafunzo ni kuhakikisha washiriki wanatekeleza kikamilifu Miongozo ya huduma za chanjo kwa kuzingatia viwango vya kitaifa sambamba na kuboresha ufuatiliaji wa huduma na kuimarisha usimamizi shirikishi kwa ngazi mbalimbali za utekelezaji.
image.png
 Ameongeza kuwa mafunzo kama hayo yalifanyika mara ya mwisho takribani miaka 10 iliyopita, na mpango uliopo sasa ni kuyafanya kila baada ya miaka mitano angalau kwa watumishi na Viongozi wapya ili kuendana na mabadiliko ya kitaalamu na mahitaji ya huduma.

Kwa upande wao baadhi ya  washiriki wa mafunzo hayo akiwemo  Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Japhet Simeo, amesema mafunzo hayo yamekuwa na umuhimu mkubwa katika kuimarisha uelewa kuhusu usimamizi wa mahitaji ya chanjo pamoja na tofauti ya vifaa vinavyotumika kuhifadhia chanjo, jambo linalosaidia kuboresha utoaji wa huduma katika vituo vya afya.
image.png
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Andrew Mathew, amesema mafunzo hayo yamewasaidia kupata mbinu bora za kuyafikia makundi maalum ya wananchi, hususan wafugaji, ili kuhakikisha wanapata huduma za chanjo kwa urahisi licha ya changamoto za kijiografia na mtindo wa maisha yao.

Katibu wa Afya wa Mkoa wa Arusha, Devotha Ntapara, pamoja na Katibu wa Afya wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leticia Mdaki, wameeleza kuwa mafunzo hayo yameongeza uelewa wao katika usimamizi wa huduma za chanjo na kuimarisha uwezo wa kupanga na kutekeleza mikakati madhubuti ya kuhakikisha chanjo zinawafikia walengwa wote kwa wakati.
image.png
Kwa ujumla, washiriki wameeleza kuwa mafunzo hayo ni chachu ya kuboresha huduma za chanjo nchini, yakilenga kuongeza ushirikishwaji, uwajibikaji na ufanisi katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya.