Na Maelezo Zanzibar 02.04.2026
Waziri wa Kazi na Uwekezaji Mhe. Shariff Ali Shariff amesema waasisi wamefanya mapinduzi makubwa katika nchi ya kuwaletea wananchi maendeleo, umoja, mshikamano na amani iliyopo.
Ameyasema hayo katika ziara ya kuwaombea dua aliekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Mstaafu Marehemu Khamis Darwesh Mdingo na Kaburi la aliyekuwa Kanal Mstaafu Marehemu Seif Bakari Omar Kiembe Samaki Wilaya ya Magharibi B.
Amesema waasisi hao wamefanya mengi mazuri kwa kuleta mapinduzi ambayo yameleta uhuru, amani na utulivu hivyo ni wajibu wa Serikali kutunza na kuendeleza Mapinduzi hayo pamoja na kuitunza historia ya nchi ili vizazi vijavyo viendelee kuisoma na kujua historia hiyo.
“Tuwashukuru na kuwaenzi wazee wetu hawa kwa neema walizozifanya na Mwenyezi Mungu awalipe kwa makubwa waliyofanya kwa ajili ya nchi yetu” ameeleza Mhe. Shariff.
Amefahamisha kuwa Wanamapinduzi hao walihitoa muhanga katika kuilinda na kudumisha umoja uliopo ambayo ni sadaka kubwa waliyotuachia.
Amesisitiza kuyaenzi, kuyaheshimu na kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar ili kuendelea umoja na mashirikiano ambayo imeifanya nchi kuwa huru katika kuleta maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake mtoto wa Marehemu Khamis Darwesh Ndugu, Asya khamis Darwesh amesema Mzee wake amesisitiza umoja na ushirikiano hivyo ameiomba Serikali kuenzi na kulinda umoja na ushirikiano huo ili nchi iendelee kuwa na amani na utulivu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Maadhimisho ya wiki ya kuwaenzi viongozi wa Kitaifa, Waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Katibu wa kwanza wa Chama cha Afro Shirazi huadhimishwa kila ifikapo April, 7 ya kila mwaka.





