Ubora na ufanisi wa huduma za chanjo unategemea moja kwa moja utunzaji sahihi wa chanjo na usimamizi madhubuti wa mahitaji yake.
Hayo yamesemwa tarehe 31, Machi,2026 Jijini Arusha na Afisa Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya Bw. Michael Ndowa wakati wa Mafunzo kwa Viongozi Wasimamizi Huduma za Chanjo (Mid-level Managers-Training ini Immunizations Services -MLM) yanayohusisha Washiriki kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
Bw.Ndowa ametoa wito kwa Washiriki kuhakikisha utunzaji sahihi wa chanjo na usimamizi madhubuti wa mahitaji yake katika vituo vya kutolea huduma.
Ndowa ameeleza kuwa kuwa ubora na ufanisi wa chanjo hutegemea kwa kiasi kikubwa namna zinavyohifadhiwa, hususan katika kuzingatia viwango sahihi vya joto.
Amebainisha kuwa chanjo nyingi zinapaswa kuhifadhiwa katika kiwango cha nyuzi joto kati ya 2°C hadi 8°C ili kudumisha nguvu yake ya kutoa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayozuilika kwa chanjo.
Amesema kuwa kutofuata taratibu hizo kunaweza kusababisha chanjo kupoteza ubora wake, hali inayoweza kuhatarisha afya ya wananchi pamoja na kudhoofisha imani ya jamii katika huduma za chanjo. “Chanjo ikiharibika kutokana na kutunzwa vibaya, madhara yake ni makubwa kwani haiwezi tena kutoa kinga iliyokusudiwa,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka washiriki kuhakikisha kuwa vifaa vya kuhifadhia chanjo, ikiwemo majokofu, vinafanya kazi kwa ufanisi wakati wote. Alisisitiza umuhimu wa kupima na kurekodi hali ya joto mara kwa mara ili kubaini mapema changamoto zozote zinazoweza kujitokeza. Pia alikumbusha juu ya ulazima wa kulinda mnyororo wa ubaridi (cold chain) kuanzia ngazi ya taifa hadi kituo cha kutolea huduma, ikiwemo wakati wa usafirishaji wa chanjo.
Katika kuimarisha upatikanaji wa chanjo, Ndowa alieleza kuwa usimamizi sahihi wa mahitaji ni muhimu ili kuepusha upungufu wa chanjo katika vituo vya afya.
Alibainisha kuwa kufanya makadirio sahihi ya mahitaji, kufuatilia matumizi na kupanga upya mahitaji kwa wakati ni hatua muhimu katika kuhakikisha huduma za chanjo zinaendelea kutolewa bila kukatika.
Kwa kuhitimisha, Ndowa alitoa wito kwa watendaji wote wa sekta ya afya kuzingatia kikamilifu miongozo na taratibu za kitaifa katika utunzaji na usimamizi wa chanjo, akisisitiza kuwa kufanya hivyo kutachangia utoaji wa huduma bora, salama na endelevu kwa wananchi, pamoja na kuimarisha kinga ya jamii dhidi ya magonjwa.





