Na Maelezo Zanzibar 31.03.2026
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Riziki Pembe Juma amesema Vituo vya Utangazaji vina nafasi kubwa katika kukuza maendeleo ya kisiasa kiuchumi na kijamii sambamba na kulinda utamaduni wa Mzanzibar.
Ameyasema hayo wakati akifunguwa semina ya siku moja kwa watendaji wa Vituo vya Utangazaji vya Zanzibar Katika Ukumbi wa ZURA ,Maisara .
Amesema mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano yameleta fursa mpya pamoja na changamoto, hivyo kuna haja kwa wadau kuwekeza katika teknolojia za kisasa, kuongeza ubunifu na kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani ili kuendana na ushindani wa kitaifa na kimataifa.
Aidha amesema kwamba umuhimu wa kutumia teknolojia si tu kurahisisha uzalishaji wa maudhui, bali pia kuhakikisha yanakuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya jamii huku yakilinda mila, silka na utamaduni wa nchi.
Amesema Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya utangazaji ikiwemo kukuza matumizi ya teknolojia za kidijitali, kuboresha mazingira ya uwekezaji, pamoja na kusisitiza uzalishaji wa maudhui ya ndani.
Amefahamisha kuwa hatua nyingine ni kufanya maboresho ya sheria, kanuni na miongozo ya utangazaji ili iendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko.
Akitoa Wito Kwa watendaji wa Vituo vya Utangazaji kuhakikisha wanaendelea kuimarisha amani na utulivu na kuakisi yale mazuri ya maendeleo ya kitaifa.
“Imarisheni Amani na utulivu mzingatie taaluma zenu haziharibu Imani ya watu na Iwe sadaka njema na iwe hadithi nzuri ya kusimuliwa Kwa vizazi i vijavyo”
Nae Mwenyekiti wa Tume ya Utangazaji Sleiman Ame Khamis amewataka wamiliki wa Vituo vya Utangazaji kuhakikisha wanajisajili na kuwa na leseni halali ya kuendeshea Vipindi sambamba na kupata hakimiliki na haki nyengine Katika Biashara yao .
Mapema Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Hijji Dadi Shajak amesema
Semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo wadau wa utangazaji katika matumizi ya teknolojia, uzalishaji wa maudhui bora na upanuzi wa masoko ili kuimarisha sekta hiyo nchini.
Amewapongeza wamiliki wa vituo vya utangazaji na wadau wote kwa kushiriki semina hiyo, akieleza kuwa ushirikiano wao ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya sekta hiyo.
Kwa Upande wa Mwenyekiti wa Muda wa Kamati ya Wamiliki wa vituo vya utangazaji Ali Mkubwa Zubeir ameiomba serikali kuwapunguzia wingi wa Kodi na kupatiwa mikopo ya kuendeshea Biashara zao
Alizitaja Miongoni mwa changamoto za Kamati hiyo ni uhaba wa matangazo Katika Vituo vyao pamoja na uhaba wa mishahada Kwa Watumishi wa Vituo hivyo
Mada mbali mbali ziliwasiliahwa ikiwemo matumizi sahihi ya akili mnemba ,uandaaji wa Vipindi Bora mambo ya kuzingatia Katika uandaaji wa mbinu za kufikia Masoko, kauli mbiu ya semina hii, “Teknolojia ya kisasa kwa maudhui bora na masoko imara”





