Silivia Amandius
Bukoba.
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi, Ndg. Kenani Kihongosi, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko la kisasa katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, mradi mkubwa unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 18.
Katika ukaguzi huo, Kihongosi amepongeza hatua iliyofikiwa ya ujenzi huku akisisitiza dhamira ya serikali ya kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia miradi ya kimkakati. Amesema soko hilo litakuwa mkombozi kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, na kuongeza kuwa litachochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa biashara na ajira katika eneo la Bukoba na mkoa mzima wa Kagera.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi huo, unaotekelezwa na kampuni ya Dimetoclasa Real Hope Limited, ujenzi ulianza Oktoba 27, 2025 na unatarajiwa kukamilika Januari 26, 2027. Hadi sasa, utekelezaji umefikia asilimia 19.45, huku kazi zinazoendelea zikihusisha maandalizi ya msingi, ujenzi wa miundombinu ya awali pamoja na usanifu wa maeneo muhimu ya soko.
Mradi huo unatarajiwa kuwa na miundombinu ya kisasa ikiwemo vizimba 1,848, maduka 234, maghala, ofisi, pamoja na huduma muhimu kama vyoo vya kisasa, mfumo wa maji safi na taka, na maeneo maalum kwa wafanyabiashara wa vyakula. Ujenzi huo unalenga kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza mapato ya wafanyabiashara pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba.
Akihitimisha ziara yake, Kihongosi amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati uliopangwa, huku akisisitiza umuhimu wa ubora wa kazi. Amebainisha kuwa serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kunufaika ipasavyo na uwekezaji unaofanywa.





