Na Silivia Amandius
Bukoba.
Msemaji na Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi mkoani Kagera kuanzia Machi 26 hadi 28 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM mkoa wa Kagera, Hamim Mahmoud, amesema ziara hiyo inalenga kuimarisha chama kwa kushuka hadi kwenye mashina na kuzungumza moja kwa moja na wanachama pamoja na mabalozi wa mashina.
Amesema pamoja na hilo, Kihongosi atakagua utekelezaji wa ilani ya CCM kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
“Lengo ni kuona kwa vitendo namna ilani ya chama inavyotekelezwa na kuhakikisha miradi hiyo inawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa,” amesema Mahmoud.
Katika ziara hiyo, Kihongosi atatembelea wilaya za Bukoba Machi 26, Muleba Machi 27 na Biharamulo Machi 28.
