Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko wa UDOM, Bi. Rose Joseph, akibadilishana mawazo na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Bi. Sekela Mwasubila, kuhusu utekelezaji wa mradi wa Huduma ya Mtandao inayotolewa kwa shule 5 na ofisi 5 za Kata.
………..
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kwa kushirikiana na UNICEF Tanzania, kimeanza kuandika ukurasa mpya wa mageuzi ya kidijitali katika Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma, kupitia utekelezaji wa mradi wa kusambaza huduma ya Mtandao kwa shule na jamii.
Katika ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo iliyofanyika Alhamisi, tarehe 19 Machi 2026, ikiongozwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko wa UDOM, Bi. Rose Joseph, imebainika kuwa hatua muhimu na ya kutia moyo tayari imefikiwa, ikiashiria mafanikio ya awali ya juhudi hizo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Msimamizi wa mradi, Dkt. Jabhera Matogoro, amesema hadi sasa vituo 10 vimeunganishwa na huduma ya intaneti yenye kasi ya 20Mbps. Vituo hivyo vinajumuisha shule tano (4 za Sekondari na 1 ya Msingi), pamoja na vituo vitano vya jamii, hatua inayotarajiwa kuleta mapinduzi katika upatikanaji wa taarifa, pamoja na kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji.
Amefafanua kuwa mradi huo unalenga kuwawezesha walimu, wanafunzi na wananchi kwa ujumla kupata maarifa kwa urahisi kupitia teknolojia ya mtandao, huku pia ukifungua milango ya fursa mpya za ajira, ubunifu wa kibiashara na maendeleo ya kijamii.
Kwa ujumla, mpango huu unaonekana kuwa kichocheo muhimu cha kupunguza pengo la kidijitali katika maeneo ya vijijini, na kuimarisha ushiriki wa jamii katika uchumi wa maarifa unaoendeshwa na teknolojia.
Miundombinu ya teknolojia ya mawasiliano ya mawimbi ya microwave inayotolewa na kampuni ya Airtel, ikisambaza huduma ya intaneti yenye kasi ya Mbps 20, kupitia Mradi unaofadhiliwa na UNICEF.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bukulu, Mwl. Joseph Paul, akieleza namna huduma ya mtandao inavyorahisisha ujifunzaji katika maabara ya kompyuta shuleni hapo.
Mkuu wa Shule ya Msingi Isabe, Mwl. Jackline Richard, akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi wa kusambaza huduma ya mtandao kwa shule na jamii.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko wa UDOM, Bi. Rose Joseph, akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Amani Abeid Karume kuhusu fursa za kujifunza kidijitali, wakati wakikagua huduma ya mtandao imavyofanya kazi shuleni hapo na kusaidia wanafunzi kujifunza.
Msimamizi Mkuu wa Mradi, Dkt. Jabhera Matogoro (Mwenye Koti), akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko wa UDOM, Bi. Rose Joseph, wakikagua matumizi ya huduma mtandao darasani kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Amani Abeid Karume iliyopo WIlayani Kondoa.
Msimamizi Mkuu wa Mradi, Dkt. Jabhera Matogoro, akitoa maelezo kuhusu utendaji wa teknolojia ya intaneti katika moja ya vituo vilivyonufaika na mradi huo, Chama cha Ushirika cha Mawasiliano.
