Afisa ushirika kutoka Halmashauri ya wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Ashura Mponda kulia,akikabidhi funguo ya gari kwa mwenyekiti wa Chama cha msingi cha ushirika Lugari Amcos Philemon Kapinga lililonunuliwa na Chama hicho kwa ajili ya shughuli za kubeba mazao ya wanachama na wakulima kama sehemu ya chanzo cha mapato,wa pili kushoto Katibu wa Ligari Amcos Cornas Kapinga.

Na Mwandishi Maalum,Mbinga

CHAMA cha msingi cha ushirika Lugari Amcos kilichopo kijiji cha Lugari kata ya Mkumbi wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,kimefanikiwa kununua gari aina ya Fuso tani saba lenye thamani ya Sh.milioni 161 litakalotumika kubeba mazao ya wanachama na wakulima kutoka mashambani na kupeleka kwenye maghala ya chama kwa ajili ya kuuzwa.

Mwenyekiti wa chama hicho Filemon Kapinga alisema,wameamua kununua gari hilo ili kurahisisha kazi ya ukusanyaji wa mazao kama kahawa inayozalishwa kwa wingi katika kata ya Mkumbi na maeneo mengine ya Wilaya ya Mbinga.

Kwa mujibu wa Kapinga,wanachama wa Lugari Amcos waliamua kubuni mradi wa gari ili kunusuru shuguli za chama kwa kukodi magari ya watu binafsi kwa bei kubwa pindi wanapataka kusafirisha mazao hususani zao la kahawa kupeleka sokoni.

Kapinga kwa niaba ya viongozi wenzake wa chama,amehaidi kulitunza gari hilo na mali nyingine za chama ili wanachama na wakulima waweze kunufaika na uwekezaji wanaofanya kupitia mazao wanayozalisha mwaka hadi mwaka na gari hilo litapunguza gharama kubwa ya usafirishaji wa mazao.

Kwa upande wake Afisa ushirika kutoka Halmashauri ya wilaya Mbinga Ashura Mponda,amewapongeza viongozi wa Lugari Amcos kwa kununua gari hilo, kusimamia chama kwa ufanisi,kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwa wakati na matumizi mazuri ya fedha za chama.

Mponda,amewataka wanachama kuhakikisha wanalitunza gari hilo ili liwasaidie kuongeza mapato ya chama chao na waendelee kushirikiana kwa karibu ili kubuni miradi mingi zaidi ya maendeleo.

Mponda,amevitaka vyama vingine vya ushirika katika Halmashauri ya wilaya Mbinga,kuiga mfano wa Lugari Amcos kununua magari ili yaweze kurahisisha ukusanyaji wa mazao kutoka mashambani kupeleka sokoni na kubuni miradi mbalimbali itakayowezesha kuongeza mapato ya vyama vyao.

Mwanachama wa Lugari Amcos Kelvin Kapinga,amewashukuru viongozi wa Amcos na wanachama kwa kubuni mradi wa gari ambalo litasaidia wanachama na wananchi wengine ambao watahitaji kukusanya na kusafirisha mazao kutoka shambani na kupeleka mjini kwa ajili ya kutafuta masoko.

Alisema,awali wanachama pindi wanapohitaji kusafirisha mazao walilazimika kuchukua magari kutoka vijiji vya jirani,hivyo kuingia gharama kubwa ambazo kwa sasa hazitakuwepo baada ya kupata gari lao.

Ameitaka bodi ya Chama kutambua kuwa,gari hilo ni gharama kubwa kwa hiyo wanatakiwa kuwa makini katika usimamizi na dereva kuhakikisha anatunza gari hilo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na lifanye kazi iliyokusudiwa.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Lugari Amcos Jackob Kapinga alisema,faida itakayopatikana kupitia gari hilo ni kurahisisha ukusanyaji na kusafirisha mazao kutoka shambani na kupeleka kwenye viwandani vya kukoboa kahawa kwa wakati.