Na Silivia Amandius.

Bukoba.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) imeendelea na juhudi za kulinda mazingira kwa kupanda miti katika vyanzo mbalimbali vya maji mkoani Kagera ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Leo march 19 mwaka huu Mhandisi Lucas Selebeya amesema hadi sasa tayari miti 1,000 imepandwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kagemu, Kaigala Muleba, Mutukula na Katoma wilayani Karagwe. Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo na kulima karibu na vyanzo vya maji, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana kulinda rasilimali hizo muhimu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyarubanja, Kata Nyanga, amepongeza juhudi za BUWASA na kuwataka wananchi kuendelea kutunza mazingira ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama unaendelea kudumu.