Mwamvua Mwinyi-Mafia

Machi 18,2026

Uvuvi haramu umekuwa tishio kubwa kwa uhai wa rasilimali za bahari na ustawi wa mazingira, huku ukichangia kupungua kwa samaki na kuathiri kipato cha jamii zinazotegemea sekta hiyo. 

Katika kukabiliana na changamoto hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mafia, mkoani Pwani Aziza Mangosongo, amekemea vitendo vya Uvuvi haramu ambapo ameitaka jamii kushirikiana pamoja na Serikllali kufichua wanaojihusisha na Uvuvi huo ili kudhibiti vitendo hivyo . 

Akizungumza wakati wa warsha ya kujengea uwezo wadau na taasisi juu ya uhifadhi na usimamizi shirikishi wa rasilimali za bahari, iliyofanyika Machi 18, 2026 Mangosongo ameeleza suala la ‘muhali’ katika jamii ni sababu kubwa inayopelekea vitendo vya uvunjifu wa sheria kuendelea.

” Sheria zimetungwa na bunge, wataalam wanavyokwenda kuwakamata wavuvi haramu, tuache sheria zifuate mkondo wake, tusilete muhali kwenye mambo ya msingi” alieleza Mangosongo

Amehimiza kila mwananchi anapaswa kutambua wajibu wake kama mhifadhi wa rasilimali za bahari na mazingira kwa ujumla.

Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu Tanzania, Emmanuel Sweke, alipongeza taasisi na vikundi vinavyojihusisha na uhifadhi wilayani Mafia na kutoa wito kwa wadau kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi na Taifa . 

Warsha hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Hifadhi za Bahari, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Taasisi ya Sayansi za Bahari, GIZ, ZMT na Chuo Kikuu cha Toliara, iliwakutanisha wataalam mbalimbali wakiwemo viongozi wa vijiji na watendaji wa kata.

Wadau hao wameahidi kuleta mabadiliko yatakayosaidia kulinda rasilimali za bahari kwa maendeleo endelevu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Juani, Ndugu Mwichande Hassan, alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutoa elimu kwa wananchi na kuomba yaendelee kufanyika mara kwa mara ili kuongeza uelewa na manufaa kwa jamii