Na John Walter-Babati

Kwa mara ya kwanza, wakazi wa Kata ya Nkaiti wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama baada ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA) kufanikisha mradi wa Darakuta–Minjingu, uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu.

Wananchi wa eneo hilo wameeleza furaha yao kubwa kwa hatua hiyo, wakisema hapo awali walikuwa wakitegemea maji yasiyo salama kutoka visima vyenye kiwango kikubwa cha madini ya floride, hali iliyokuwa ikiathiri afya na maisha yao kwa ujumla.

Mkazi wa Nkaiti, Maria Chambia, amesema kina mama walikuwa wakipata shida kubwa kutafuta maji, wakilazimika kutembea umbali mrefu nyakati za usiku wakiwa na ndoo na vyombo vya kuhifadhia maji.

“Nguzo kubwa ya changamoto ilikuwa maji. Tulitumia maji yaliyoharibu hata nguo zetu, usafi ulikuwa mgumu. Mama unakuwa mchafu kuanzia asubuhi hadi jioni. Sasa mazingira yatakuwa safi na bora zaidi. Mungu ambariki Rais wetu Mama Samia,” amesema Maria.

Naye Lembris Zakaria amesema kuwa tangu akiwa kijana walikuwa wakisikia tu kuhusu upatikanaji wa maji safi katika maeneo mengine, lakini kwa sasa ndoto hiyo imetimia.

“Tuna furaha sana. Tunaomba tu huduma hii iwe ya kudumu bila mgao, maana sasa tunaweza hata kuvuta maji hadi majumbani kwetu,” amesema.

Kwa upande wake, Kiongozi wa kimila wa Malaigwanani, Chifu Lobulu Leteiva, ameishukuru serikali pamoja na viongozi wa eneo hilo kwa juhudi zilizowezesha kufanikisha mradi huo.

Pia ameomba kutengwa kwa maeneo maalum kwa ajili ya kunyweshea mifugo ili kuepusha migongano ya matumizi ya maji.

Diwani wa Kata ya Nkaiti, Steven Saruni Mollel, amesema mradi huo ulikuwa ndoto ya muda mrefu tangu miaka ya 1980, lakini hatimaye umefanikishwa chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

“Huu ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wetu. Serikali ya Rais Samia imetoa fedha na sasa wananchi wanaanza kuona matokeo halisi,” amesema.

Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Maji, Mkurugenzi Mtendaji wa BAWASA, Mhandisi Iddy Msuya, amesema zaidi ya wananchi 35,000 watanufaika na huduma hiyo baada ya kukamilika kwa mradi wa Darakuta–Minjingu.

Ameeleza kuwa mradi huo umegharimu takribani shilingi bilioni 16 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita, na kuutaja kuwa ni mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Nkaiti ambao kwa muda mrefu hawakuwa na huduma ya maji safi na salama.

Naye Meneja wa Huduma kwa Wateja, Rashid Chalahani, amesema huduma ya maji itaanza kutolewa rasmi, huku akiwahamasisha wananchi kujiunga na huduma hiyo kwa kuvuta maji majumbani mwao.

Ameongeza kuwa kutakuwa na ofa maalum kwa wateja wapya ambapo wananchi watalipia gharama za vifaa pekee, na kuunganishiwa huduma ndani ya wiki moja baada ya kukamilisha malipo.

Mradi huo unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi katika Kata ya Nkaiti, ikiwemo kuboresha afya, usafi wa mazingira, na kuongeza muda wa wananchi kushiriki shughuli za maendeleo badala ya kutafuta maji.