Na Farida Mangube, Morogoro
Serikali imeuagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuandaa mpango na mkakati madhubuti wa kuwezesha makundi mbalimbali mkoani Morogoro kuzalisha nishati safi ya kupikia kwa kutumia pumba za mchele. Hatua hiyo inalenga kupunguza gharama za uzalishaji, kunusuru misitu na mazingira, pamoja na kulinda afya za Watanzania.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati wa ufunguzi wa kongamano la kuboresha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa maendeleo endelevu nchini, lililofanyika mkoani Morogoro.
Kongamano hilo liliwakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar, na kuandaliwa na Taasisi ya Uongozi (UONGOZI Institute).
Akifungua kongamano hilo, Waziri Ndejembi alisema kuwa uwezeshaji wa makundi hayo utaongeza kasi ya wananchi kuachana na matumizi ya nishati chafu na kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia, hatua itakayochochea pia ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Aidha, Waziri huyo alibainisha kuwa serikali imeondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye uagizaji wa mitungi ya gesi na vifaa vya kuchakata mkaa mbadala (carbonizers), kwa lengo la kupunguza gharama na kurahisisha upatikanaji wa nishati safi kwa wananchi.
Aliongeza kuwa kupitia mkakati wa taifa wa mawasiliano ya nishati safi ya kupikia, serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya kutumia nishati chafu na faida za nishati safi. Alisema kampeni hiyo tayari imeanza katika mikoa ya Tanga, Dodoma, Morogoro na Njombe, na itaendelea nchi nzima.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Bw. Kadiri Singo, alisema kongamano hilo lina lengo la kujadili njia bora za kuhamasisha na kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza athari za kiafya, kulinda mazingira na kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yana mchango mkubwa katika kuboresha afya, kupunguza uharibifu wa misitu na kupunguza uzalishaji wa gesi chafu zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Adam Kighoma Malima, alisema mkoa huo umeanza kuweka mikakati ya kutoza ushuru wa shilingi 20,000 kwa kila gunia la mkaa unaotokana na miti, ili kudhibiti biashara hiyo na kulinda misitu.
Aliongeza kuwa uwekezaji katika kuongeza thamani ya pumba za mpunga kwa ajili ya kutengeneza mkaa mbadala utawawezesha wananchi wa Morogoro kushiriki kikamilifu katika mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

