NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amefungua rasmi kongamano la wadau wa habari, wahariri na waandishi wa habari la mwaka 2026 (MISA TAN Summit), akisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Kheri James alianza kwa kumshukuru Mungu kwa uzima, afya na fursa ya kushiriki katika tukio hilo kubwa linalobeba historia kwa Mkoa wa Iringa alieleza kuwa ni heshima kubwa kwa mkoa huo kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa unaowakutanisha wadau wa habari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Alibainisha kuwa vyombo vya habari vina jukumu muhimu la kuhabarisha, kuelimisha umma na kuchochea mijadala ya maendeleo, hivyo uwepo wa wataalamu wa sekta hiyo Iringa ni ishara ya dhamira ya pamoja ya kujenga taifa lenye maendeleo endelevu.
Mkuu huyo wa mkoa aliutangaza Mkoa wa Iringa kuwa ni eneo lenye mazingira rafiki kwa uwekezaji, akitaja mafanikio katika ukusanyaji wa mapato ambapo mkoa umeendelea kuvuka malengo kila mwaka. Aliwapongeza wafanyabiashara, wakulima, wafugaji na wananchi kwa ujumla kwa mchango wao katika kukuza uchumi wa mkoa na taifa.
Katika sekta ya elimu, alisema mkoa una shule nyingi za msingi na sekondari pamoja na vyuo vya elimu ya juu na kati, huku serikali ikiendelea kuwekeza ili kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa wote.
Aidha, alieleza kuwa huduma za afya zimeboreshwa kwa kuongeza vituo vya kutolea huduma, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi.
Kuhusu miundombinu, Kheri James alisema mkoa una mtandao mpana wa barabara unaounganisha maeneo ya uzalishaji mali, huku vijiji vyote vikiwa vimefikiwa na huduma ya umeme. Pia alitaja maboresho ya Uwanja wa Ndege wa Nduli kuwa yameongeza fursa za biashara, utalii na usafiri wa anga.
Aligusia pia jitihada za serikali katika kukuza sekta ya utalii, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na ujenzi wa kituo cha taarifa za utalii kitakachorahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wageni na wawekezaji.
Kwa upande wa kilimo, Mkuu huyo wa mkoa alisema serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miradi ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha wakulima wanapata tija zaidi.
Awali akizungumza, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kuunga mkono kongamano hilo. Alisema MISA Tanzania inaendelea kusimamia uhuru wa vyombo vya habari na kukuza uwandishi wa habari wa suluhisho (constructive journalism) unaolenga kuibua changamoto pamoja na kutoa majibu yake.
Alieleza kuwa kongamano hilo limewakutanisha wahariri na waandishi wa habari kutoka ndani na nje ya nchi, likiwa na lengo la kujadili mchango wa vyombo vya habari katika maendeleo ya taifa na kuhamasisha utoaji wa taarifa zenye kujenga jamii.
Soko aliongeza kuwa MISA Tanzania pia ina mpango wa kuanzisha kituo cha mawasiliano kwa jamii (community telecenter) kitakachosaidia wananchi kupata taarifa muhimu za maendeleo ikiwemo bei za mazao, hali ya hewa, fursa za kiuchumi na matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali katika mkoa Iringa.
Katika kuanzisha kituo cha kanda ya nyanda mkuu wa mkoa wa Iringa James amewakubalia misa kuwapatia eneo la kujenga kituo hicho.

