Na Silivia Amandius 

Bukoba.

Hatimaye jitihada za muda mrefu za wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Bunena, Manispaa ya Bukoba, zimezaa matunda baada ya kupatikana mashine ya kudurufu mitihani (photocopy) yenye thamani ya shilingi milioni 3.4.

Awali, wazazi walichangishwa fedha kwa lengo la kununua mashine hiyo, lakini mchakato huo ulichukua takribani miaka mitano bila mafanikio. Hali hiyo ilisababisha wanafunzi kuchelewa kuzoea mitihani iliyochapishwa, jambo lililoathiri maandalizi yao ya kitaaluma kwa muda mrefu.

Kupatikana kwa mashine hiyo Machi 17 kumetokana na ushirikiano kati ya Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhandisi Johnstone Mtasingwa, Diwani wa Kata ya Bakoba Shabani Rashidi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo. Wazazi na walezi wameeleza furaha yao na kumpongeza mbunge huyo kwa kutimiza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni.

Kupitia kwa Katibu wake, Hamada Simba, mbunge huyo amekiri kupokea pia ombi la kompyuta mbili kwa ajili ya kuchapisha mitihani, na kuahidi kuzitoa kwa haraka ili kuboresha zaidi mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Diwani wa Kata ya Bakoba, Shabani Rashidi, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya ofisi yake na ofisi ya mbunge, akisema hatua hiyo ni sehemu ya mafanikio ya kushughulikia changamoto za wananchi ndani ya muda mfupi.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Devotha Mugisha, amesema upatikanaji wa mashine hiyo pamoja na vifaa vya TEHAMA utasaidia kuimarisha matumizi ya teknolojia shuleni hapo, kuongeza ufanisi wa utoaji mitihani na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuzoea mfumo wa mitihani ya kisasa. Ameongeza kuwa hatua hiyo itaongeza ufaulu na kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kujiunga na shule za vipaji maalum.