

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda (kushoto) akitoa ufafanuzi wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) leo Machi 17, 2026 jijini Dar es Salaam.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya akitoa ufafanuzi wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila, leo Machi 17, 2026 jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Husna Juma Sekiboko akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kamati hiyo kuridhishwa na utendaji wa utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) MUHAS.



kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakikagua utekelezaji wa miradi katika ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)
…………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amepongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa juhudi za kuendeleza Kampasi ya Mloganzila kuwa mji wa kitaaluma na tiba.
Amesema kampasi hiyo itajumuisha vituo vya umahiri vitakavyotoa huduma za matibabu, elimu na utafiti kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya pamoja na elimu ya juu nchini.
Akizungumza leo Machi 17, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo, Prof. Mkenda ameeleza kuwa ujenzi unaoendelea unahusisha majengo ya hosteli, ukumbi wa mihadhara, maabara changamano, kantini, utawala, TEHAMA pamoja na maktaba.
Prof. Mkenda amebainisha kuwa Serikali imetenga dola za Marekani milioni 83 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali maalum ya tiba, ambayo itakuwa sehemu ya kituo hicho. Hospitali hiyo itasaidia kutoa mafunzo kwa vitendo, kufanya tafiti, na kuhudumia wagonjwa.
Amesisitiza kuwa lengo ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha taaluma za tiba katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, sambamba na kuzalisha wataalamu na wabobezi wa kutosha kuhudumia Watanzania pamoja na wageni wanaokuja kupata huduma za afya.
Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila ya MUHAS.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Husna Juma Sekiboko, amekipongeza chuo hicho kwa usimamizi mzuri wa mradi, akibainisha kuwa utekelezaji wake uko mbele kwa zaidi ya asilimia 10 ukilinganishwa na mkataba.
Mhe. Sekiboko amesema MUHAS inapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika usimamizi wa miradi ya ujenzi ikilinganishwa na taasisi nyingine za elimu ya juu.
Ameongeza kuwa mradi huo utaleta manufaa makubwa, ikiwemo kuongeza udahili wa wanafunzi, kuboresha mazingira ya kujifunzia, na kuongeza idadi ya madaktari ambao kwa sasa hawatoshelezi mahitaji yaliyopo.
Amefafanua kuwa mradi huo unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 115, fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Naye Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya, amesema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha utoaji wa huduma katika sekta ya afya na kuongeza nafasi za udahili kwa wanafunzi.
Ameeleza kuwa jengo la utawala la Ndaki ya Tiba lina uwezo wa kuhudumia watu 450 kwa wakati mmoja, huku maktaba na kituo cha TEHAMA vikitarajiwa kuhudumia watumiaji 550 kwa wakati mmoja.
Aidha, amebainisha kuwa miundombinu muhimu ya kampasi hiyo itajumuisha uwanja wa mpira wa miguu pamoja na barabara za kuunganisha majengo mbalimbali.
