Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua huduma mpya ya intaneti ya Faiba Mlangoni Kwako – Supersonic Experience; Kasi Balaa, hatua inayolenga kuongeza kasi ya mageuzi ya kidijitali nchini na kuwezesha wananchi kupata huduma ya intaneti yenye ubora, uhakika na gharama nafuu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo jana Machi 16, 2026, Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Vedastus Mwita, alisema huduma hiyo ni sehemu ya juhudi za shirika hilo kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kuwafikia Watanzania wengi zaidi katika enzi ya uchumi wa kidijitali.
Mwita, alisema tukio hilo linaashiria hatua muhimu katika safari ya mageuzi ya kidijitali nchini, huku TTCL ikiendelea kuwa kinara katika kuleta ubunifu, kuboresha miundombinu ya mawasiliano na kufungua fursa mpya za mawasiliano kwa Watanzania.
“Leo hatujakusanyika tu kwa ajili ya tukio la uzinduzi, bali kushuhudia hatua muhimu inayoongeza kasi ya mageuzi makubwa ya teknolojia ya mawasiliano nchini. TTCL imeendelea kuongoza juhudi za kuleta ubunifu na kuboresha miundombinu ili kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi zaidi,” alisema Mwita.
Alisema katika dunia ya sasa ya kidijitali, intaneti yenye kasi, ubora na uhakika imekuwa mhimili muhimu wa kuendesha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi zikiwemo biashara, elimu, afya pamoja na ubunifu wa vijana.
Kwa mujibu wa Mwita, upatikanaji wa intaneti ya uhakika na yenye gharama nafuu si anasa tena, bali ni hitaji la msingi katika kuendeleza uchumi wa taifa. Hivyo TTCL imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hizo.
Alifafanua kuwa huduma ya Faiba Mlangoni Kwako – Supersonic Experience inalenga kuwapa wateja uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa kama vile Smart Home, Smart Office, biashara mtandaoni, michezo ya mtandaoni pamoja na huduma za (streaming) bila usumbufu wa kasi ndogo ya intaneti.
“Huduma hii imeboreshwa kwa kasi ya juu sana itakayomwezesha mteja kufanya shughuli zake za kidijitali bila wasiwasi wowote. Tunahakikisha kila mteja anapata uzoefu bora zaidi wa intaneti,” alisema.
Katika uzinduzi huo, TTCL ilitangaza vifurushi vipya vya huduma ya T-Fiber Supersonic Experience, ambavyo ni:
T-Fiber Busta – Kasi ya 60/60 Mbps pamoja na dakika 250 za simu ya mezani kwa Sh55,000 kwa mwezi., T-Fiber Triple Hub Plus– Kasi ya 100/100 Mbps, dakika 300 za simu ya mezani na GB 20 za mawasiliano ya simu ya mkononi kwa Sh70,000 kwa mwezi. Mteja atapata laini moja ya simu ya TTCL bure, T-Fiber Triple Hub Extra– Kasi ya 150/150 Mbps, dakika 700 za simu ya mezani na GB 30 za mawasiliano kwa Sh100,000 kwa mwezi, pamoja na laini mbili za TTCL bure.
Vifurushi vingine ni T-Fiber Triple Hub Balaa– Kasi ya 200/200 Mbps, dakika 1,200 za simu ya mezani na GB 40 za mawasiliano kwa Sh150,000 kwa mwezi, pamoja na laini tatu za TTCL bure na T-Fiber Triple Hub Jumbo – Kasi ya 250/250 Mbps, dakika 2,500 za simu ya mezani na GB 50 za mawasiliano kwa Sh200,000 kwa mwezi, pamoja na laini tatu za TTCL bure.
Mwita alisema wateja watakaojiunga na vifurushi hivyo pia watapata ofa ya laini za simu za mkononi za TTCL bila gharama kulingana na kifurushi walichochagua.
Aliongeza kuwa kupitia vifurushi hivyo vipya, wateja wataweza kufanya shughuli nyingi za kidijitali kwa ufanisi zaidi ikiwemo ku-stream video za ubora wa juu, kucheza michezo ya mtandaoni, kupakua na kupakia taarifa kwa haraka pamoja na kutengeneza na kusambaza maudhui ya kidijitali kwa urahisi.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kutumia huduma za mawasiliano zenye ubora na usalama, zitakazochochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” alisema.
Alisisitiza kuwa TTCL itaendelea kuboresha huduma zake ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wateja katika kipindi hiki cha mapinduzi ya kidijitali, huku akibainisha kuwa maboresho zaidi ya huduma za mawasiliano bado yanaendelea kufanyika nchini.

