Mbunge wa Jimbo la Segerea kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Mhe. Agnesta Kaiza (wa kwanza kushoto) akikabidhi Leo Machi 16, 2026 mahitaji   muhimu ya kila siku ikiwemo mchele, unga wa sembe, unga wa ngano, mafuta ya kupikia, sabuni za unga na za miche katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Mwana Orphanage Centre kilichopo Kata ya Vingunguti, Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuwafariji na kuwapa mkono wa heri watoto hao kuelekea katika  sikukuu za Iddi na Pasaka.

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

……..

Mbunge wa Jimbo la Segerea kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Mhe. Agnesta Kaiza, ametembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali muhimu katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Mwana Orphanage Centre. huku akiahidi kushughulikia changamoto inayowakabili watoto wa kituo hicho kuhusu madai ya kuzulumiwa nyumba yao waliokuwa wakiishi awali.

Msaada uliotolewa na Mbunge huyo unajumuisha mahitaji muhimu ya kila siku ikiwemo mchele, unga wa sembe, unga wa ngano, mafuta ya kupikia, sabuni za unga na za miche, miswaki, dawa ya meno, madaftari, kalamu, juisi, chumvi, sukari pamoja na maharage. Aidha, Mhe. Kaiza alitoa kiasi cha shilingi laki mbili (200,000) kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa mboga mboga.

Msaada huo umetolewa kama sehemu ya kuwafariji na kuwapa mkono wa heri watoto hao kuelekea katika  sikukuu za Iddi na Pasaka.

Akizungumza leo Machi 16, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi msaada huo katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Mwana Orphanage kilichopo Kata ya Vingunguti, Mhe. Kaiza aliupongeza uongozi wa kituo hicho kwa juhudi wanazozifanya katika kuhakikisha watoto yatima wanapata malezi bora, upendo na huduma muhimu zinazowasaidia kukua katika mazingira salama na yenye matumaini.

Mhe. Kaiza amesisitiza umuhimu wa jamii kwa ujumla kuwa na moyo wa kujali na kusaidia watoto yatima pamoja na makundi mengine yenye uhitaji maalum.

Amesema ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kuhakikisha watoto hao wanapata fursa sawa za maisha, elimu na maendeleo ili waweze kufikia ndoto na malengo yao ya baadaye.

Akizungumzia changamoto ya madai ya kunyimwa au kuzulumiwa nyumba waliokuwa wakiishi watoto hao, Mhe. Kaiza amesema yupo tayari kufuatilia suala hilo kwa karibu kwa kushirikiana na uongozi wa kituo hicho pamoja Serikali za mtaaa ili kuhakikisha haki inapatikana.

“Kuhusu changamoto ya kuzulumiwa nyumba, nitakaa na uongozi wa kituo hiki ili wanipatie taarifa zote kwa kina. Baada ya hapo nitafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha haki inapatikana kwa watoto hawa,” amesema Mhe. Kaiza.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Mwana Orphanage, Bi. Sada Omary Ally, amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Segerea kwa msaada huo mkubwa alioutoa, akieleza kuwa utasaidia kupunguza changamoto za mahitaji ya msingi kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho.

Naye mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho, Naifat Nassor, ametoa ombi kwa Mbunge huyo kusaidia kufuatilia haki yao kuhusu nyumba waliyoondolewa, huku akieleza kuwa awali watoto hao walikuwa wakiishi katika nyumba hiyo, lakini kwa sasa wamelazimika kupanga nyumba nyingine.

Kutokana na hali hiyo, kituo hicho kinapaswa kulipa kodi ya nyumba ya kiasi cha shilingi laki tano (500,000) kila mwezi, jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa kituo hicho.