NA DENIS MLOWE, IRINGA
KATIBU wa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Yahaya Mpelembwa, ametembelea eneo la tukio la moto lililotokea usiku wa kuamkia jana katika Garden Masai Market, na kutoa pole kwa zaidi ya wafanyabiashara 20 waliopoteza mali zao.
Mpelembwa alimwakilisha mbunge wa jimbo hilo, Fadhili Fabian Ngajilo, ambaye hakuweza kufika kutokana na majukumu ya vikao vya kamati.
Moto huo ulizuka kati ya saa 5:00 usiku na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali katika mabanda ya wafanyabiashara, wengi wao wakiwa wanajishughulisha na shughuli zinazohusiana na utalii.
Zaidi ya wafanyabiashara 50 walikuwapo eneo hilo wakati tukio lilipotokea, na juhudi za wananchi, Jeshi la Polisi na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya zilisaidia kuzuia madhara kuwa makubwa zaidi.
Akitoa salamu za pole kutoka kwa mbunge, Mpelembwa alisema ofisi ya mbunge inaendelea kufuatilia kwa karibu tathmini ya athari za tukio hilo, ikiwemo kubaini chanzo cha moto na thamani ya mali iliyoharibika.
Aliwataka wafanyabiashara kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu na kusisitiza kuwa taarifa za kupotosha kuhusu hatma ya eneo hilo hazitoki serikalini wala kwa viongozi wa maeneo.
Aliongeza kuwa baadhi ya waathirika ni wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, na kuwahakikishia kuwa ofisi ya mbunge itaendelea kusimama nao ili kuhakikisha wanarejea katika shughuli za uzalishaji kupitia usimamizi na maboresho ya miundombinu ya maeneo ya biashara.
Aidha, Mpelembwa alisema kuwa mara tu mbunge atakaporejea, atatembelea eneo hilo ili kuungana na wafanyabiashara hao na kujadili hatua za msaada zitakazowezesha kurejesha biashara zao.
Akihitimisha ziara hiyo, Mpelembwa aliwatia moyo wahanga kwa kuwaambia kuwa “kuteleza si kuanguka,” na kuwataka waendelee kuwa na matumaini ya kurejea katika hali nzuri zaidi ya kiuchumi baada ya tathmini na taratibu za msaada kukamilika.
Viongozi wa eneo hilo pia wamewataka wananchi na wafanyabiashara kutokuwa waoga kutokana na uvumi unaoenea kuhusu uwezekano wa kuondolewa katika eneo hilo. Wamesema kuwa endapo kungekuwa na taratibu zozote rasmi, wananchi wangejulishwa mapema.
Katika tukio hilo, baadhi ya wahanga wametajwa kuwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri.
Ofisi ya Mbunge imetoa tahadhari kwao kutokata tamaa au kuogopa kurejesha mikopo hiyo kwa sababu hata mamlaka husika zinatambua changamoto iliyojitokeza.
Uongozi wa eneo umeahidi kuendelea kukusanya taarifa za kitaalamu kuhusu athari halisi za moto, thamani ya mali iliyopotea, na hatua za msaada zitakazochukuliwa kwa kushirikiana na mamlaka husika.

