Na Neema Mtuka
Sumbawanga
Rukwa :Mkoa wa Rukwa unaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kupitia maadhimisho yaliyoandaliwa na Plan International, yakilenga kuwawezesha wanawake na wasichana pamoja na kutambua mchango wao katika maendeleo ya jamii.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo mwakilishi kutoka Plan International Bi. Christina Luhanda ameainisha Kupitia miradi mbalimbali, zaidi ya watoto 13,857 wananufaika na programu za elimu ya jinsia kwa vijana, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, pamoja na uwezeshaji wa vikundi vya vijana na wanawake kupitia mikopo na shughuli za kiuchumi.
Katika maadhimisho hayo, wanawake vinara kutoka vikundi na watu binafsi wanatambuliwa na kupatiwa tuzo pamoja na vifaa vya kuwaongezea thamani katika shughuli zao za uzalishaji na biashara.
Mgeni rasmi ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Peter Lijualikali, anayemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa huku wadau wakihimiza kuendelea kuimarisha ulinzi wa haki za wanawake na wasichana pamoja na kuongeza fursa za ajira zenye staha.
Sambamba na hilo pia Lijualikali ameahidi kushirikiana na shirika la Plan International ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Aidha amewataka wanawake kuendelea kujitokeza katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwa kuwa wanaweza.
Nao baadhi ya wanawake waliojitokeza katika maadhimisho hayo akiwemo Rose Mwesa ameitaka jamii kutowatenga wanawake hasa wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi.
“Kuna baadhi ya watu huwatenga wanawake kwa kuwasema vibaya hasa wale wanaowania nafasi za uongozi,wote tunahaki sawa na tunapaswa kushiriki katika nyadhifa mbalimbali.” Amesema Mweso

