Mtendaji wa Kata ya Mecco Masunga Mpandachalo akisoma taarifa ya ujenzi wa zahati kwa kamati ya siasa.
Mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Nyamwilekelwa iliyopo kata ya Mecco Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza.
Wajumbe wa kamati ya siasa wakikagua ujenzi wa zahanati ya Mecco.
Muonekano wa jengo la Zahanati ya Mecco ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 45 
………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza wametembelea na kukagua miradi miwili ya maendeleo ili waweze kujiridhisha kama fedha zinazotolewa na serikali zinatumika ipasavyo.
Kamati hiyo imetembelea mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Nyamwilekelwa pamoja na jengo la zahanati ya Mecco.
Akizungumza baada ya kutembelea miradi hiyo Mwenyekiti wa CCM kata ya Mecco, Naomi Luzunya amewataka wasimamizi wa miradi hiyo kusimamia vizuri ili thamani ya fedha iweze kuonekana kwakutekeleza miradi yenye ubora ambayo italeta tija kwenye jamii.
“Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya afya hivyo fedha zinapoletwa inatakiwa mzisimamie vizuri ili ziweze kuleta matokeo chanya”,
Akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo la Zahanati hiyo Mtendaji wa kata ya mecco, Masunga Mpandachalo amesema mradi huo hadi kukamilika utagharimu milioni 75 na hadi sasa umefikia asilimia 45.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Nyamwilekelwa Mwalimu mkuu wa Shule hiyo, Fatna Bagoka amesema walipokea milioni 25 kwaajili ya ukamilishaji wa ujenzi huo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mecco, William Bulugu amesema mradi wa ujenzi wa zahanati ya Mecco utakapokamilika utawasaidia wananchi kupata huduma za afya karibu.
Amesema kwa miaka mingi wananchi hao wamekuwa wakienda kupata huduma za afya katika maeneo jirani ikiwemo zahanati ya Buzuruga.