Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Kisare Makoria,akizungumza jana baada ya kukabidhi msaada wa chakula aina mbaimbali kwa Shehe wa wilaya hiyo Said Majidu kwa ajili ya futari kwa waumini wa dini ya kiislamu ambao wako kwenye mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan,kulia Katibu Tawala Pendo Daniel Ndumbaro na kushoto viongozi wa dini hiyo(Picha na Muhidin Amri),

Na Mwandishi Wetu,Mbinga

WAUMINI wa Dini ya Kiislamu na wananchi wa wilaya ya Mbinga kwa ujumla,wametakiwa kuendelea kufanya mambo mema yanayompendeza Mungu ikiwemo kudumisha amani,utulivu na kufanya Ibada katika kipindi hiki na baada ya kumalizika kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kisare Makori,wakati akikabidhi msaada wa vyakula vya aina mbalimbali kwa viongozi wa dini ya kiislamu kwa ajili ya futari kwa waumini wa dini hiyo wanaoendelea na mfungo wa Ramadhan.

“Napenda kuwapongeza wenzetu wa dini ya kiislamu kutekeleza moja ya nguzo kubwa ya mwezi mtukufu wa Ramadhan,tunavyoelewa mwezi huu ni moja ya msingi muhimu sana kwa wenzetu waislamu”alisema Makori.

Makori alisema,wananchi wa wilaya ya Mbinga wameendelea kuishi kwa upendo,amani,utulivu na ushirikiano bila kubaguana kutokana na tofauti zao za dini.

Makori ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama katika Wilaya ya Mbinga,amewataka waislamu kuhakikisha mambo mema wanayofanya katika kipindi hiki isiwe mwisho wao hata baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani.

Makori,amewashukuru wananchi wa Mbinga kwa kuendelea kudumisha amani,kuishi kwa upendo kama jamii moja na kutumia muda wao katika kufanya kazi za kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na wilaya ya Mbinga kwa ujumla.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo wa chakula, Shehe wa wilaya ya Mbinga Said Majidu,amemshukuru Mkuu wa wilaya kutoa msaada huo ambao utasaidia waumini waliopo kwenye mfungo wa Ramadhan kupata futari.

Kwa mujibu wa Shehe Majidu,vyakula hivyo vitawanusuru watu wanaosimamia waislamu katika mazingira ya aina mbalimbali kwani hawapeleki majumbani mwao badala yake watapeleka kwa watu wenye mahitaji ambao hawana uwezo wa kupata futari.

 Amewataka waislamu kuendelea kuwaombea viongozi na nchi yetu iwe na amani kwani bila amani na utulivu hatuwezi kufanya jambo lolote la maendeleo.

Alisema kuwa,neema zilizopo nchini za amani na maendeleo yanayofanywa na kusimamiwa na viongozi wakuu ni jambo linalopaswa kuenziwa na kusimamiwa na kila mwananchi ili Mungu azidi kuwazidishia neema,baraka na kuwatia moyo viongozi wetu kama dini inavyoelekeza.

Shehe Majidu alisema,maandiko katika vitabu vitakatifu vinaeleza umuhimu wa kudumisha umoja,upendo na mshikamano baini ya waumini,hivyo amewasihi waumini kuacha kudharauliana na kubezana ili kuepusha kutokea ugomvi na mifarakano miongoni mwao.

Amewataka wazazi na walezi wilayan Mbinga, kuwasimamia vijana wao katika maadili na kuwapatia elimu zote mbili ya dunia na akhera kwa manufaa yao wenyewe na Taifa kwa ujumla jambo ambalo litapelekea kupata viongozi bora wa serikali pamoja na viongozi watakaosimamia dini yao.

Aidha,amewataka waislamu kuondoa tofauti zao za kidunia na kushirikimana katika kufanya Ibada ili kufikia lengo la kuumbwa kwao hapa duniani kama alivyofanya Mtume Muhammad(S,A,W) ambaye ni kigezo cha waumini wa dini ya kiislamu ambao wanapaswa kufuata nyayo zake.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa wilaya ya Mbinga Pendo Daniel Ndumbaro,ametaja baadhi ya vyakula vilivyokabidhiwa ni gunia nne za mchele za ujazo wa kilo 100 kila moja,gunia mbili za maharage,unga wa ngano mifuko mwili,sukari katoni tatu na boksi mbili za tende kwa ajili ya waumini wa kiislamu.

Ndumbaro alisema,ofisi ya mkuu wa wilaya imeona ni vema kutoa msaada wa vyakula ili kuwapa faraja waumini wa dini hiyo ambao wanaendelea kutekeleza moja ya nguzo muhimu ya dini yao.

“Kuna baadhi ya watu wako kwenye mfungo wa Ramadhan lakini hawana uwezo wa kupata futari na mahitaji mengine muhimu, kwa hiyo kufanya hivyo tutakuwa tumeshiriki kwa namna moja au nyingine kutenda matendo mema yanayompendeza Mungu”alisema Ndumbaro.