NA DENIS MLOWE IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini,Fadhil Ngajilo ameishauri serikali kuongeza msukumo katika utekelezaji wa miradi muhimu ya maendeleo katika Manispaa ya Iringa, ikiwemo ujenzi wa soko la Machinga Complex ambalo ni ahadi iliyotolewa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika kikao cha Wasilisho la Bajeti ya Mkoa ya mwaka 2026/2027 kwenye Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) mbunge Ngajilo alisema ni muhimu kusisitiza miradi ambayo inahitaji msukumo zaidi ili iweze kuanza au kuharakishwa utekelezaji wake.
Alisema moja ya miradi hiyo ni ujenzi wa soko la Machinga Complex ambalo liliahidiwa na Rais na linatarajiwa kwa hamu kubwa na wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga katika mji wa Iringa.
Alieleza kuwa hadi sasa hajaliona soko hilo likitajwa kwa kina katika mipango ya jumla ya masoko, jambo linalozua wasiwasi kwa wananchi wanaosubiri utekelezaji wa ahadi hiyo muhimu.
Mbunge huyo alisema Manispaa ya Iringa tayari imeshatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo katika eneo la stendi ya zamani ya mabasi, hivyo kinachohitajika sasa ni kuanza majadiliano na taratibu za utekelezaji wa mradi huo.
Alisisitiza kuwa kwa kuwa ni ahadi ya Rais, wananchi wanategemea kuona hatua za utekelezaji zikianza mapema ili kuondoa sintofahamu na kuleta matumaini kwa wafanyabiashara wanaosubiri soko hilo.
Mbali na suala la soko la machinga, mbunge huyo pia aliomba jitihada za Manispaa ya Iringa katika ujenzi wa shule za English Medium zitambuliwe.
Alisema manispaa imeanza ujenzi wa shule tatu za aina hiyo, ambapo baadhi zimekamilika na nyingine zinaendelea kujengwa.
Aliongeza kuwa ni muhimu taarifa hizo ziwekwe wazi katika ripoti za maendeleo ili wananchi na wadau waweze kuona juhudi zinazofanywa na halmashauri katika kuboresha sekta ya elimu.
Katika hatua nyingine, mbunge huyo alizungumzia ujenzi wa daraja la Isakalilo linalounganisha maeneo ya Isakalilo, akisisitiza kuwa daraja hilo ni muhimu kwa maendeleo ya mkoa wa Iringa na linahitaji kupewa kipaumbele katika mipango ya serikali.
Alisema awali serikali ilitoa majibu kuwa kuna mpango wa kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo, hivyo viongozi wa mkoa wanapaswa kuendelea kuweka msukumo ili mradi huo uingizwe rasmi katika taratibu za utekelezaji.
Aidha, aligusia pia suala la eneo la Magereza lililopo karibu na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, akisema kwa muda mrefu kumekuwa na mazungumzo kuwa magereza yatahamishiwa eneo la Mlolo.
Alisema taarifa zinaonyesha eneo la Mlolo tayari lilitengwa kwa ajili ya shughuli za magereza na hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa huko, lakini bado haijawekwa wazi kama magereza ya zamani yamehama kabisa au bado yanaendelea kutumia eneo hilo.
Kutokana na hali hiyo, aliomba ufafanuzi wa wazi utolewe ili wananchi waelewe hatima ya eneo hilo, kwani bado kuna shughuli zinazoonekana kuendelea katika eneo la magereza ya zamani.
Mbunge huyo alieleza kuwa iwapo eneo hilo litakuwa wazi, linaweza kutumika kupanua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa ambayo kwa sasa ina eneo finyu lisilotosha kukidhi mahitaji ya huduma za afya kwa wananchi.
Alisema upanuzi wa hospitali hiyo ni muhimu ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Iringa na mikoa jirani wanaotegemea hospitali hiyo kupata matibabu ya rufaa.
Aliongeza kuwa masuala aliyoyataja kuhusu manispaa ni yale yanayohusu halmashauri moja kwa moja, lakini pia yapo mengine ya ngazi ya mkoa ambayo yanahitaji kushughulikiwa na mamlaka za juu zaidi.