Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa:Zaidi ya wananchi elfu 45 mkoani Rukwa wanatarajiwa kunufaika na mpango wa bima ya afya bure unaolenga kuwasaidia kupata huduma za matibabu bila gharama.
Akizungumza katika semina aliyoiandaa kwa viongozi wa umoja wa wanawake mkoani Rukwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, Jacqueline Mzindakaya, amesema tayari wananchi zaidi ya 22,000 wamesajiliwa katika mpango huo, huku zoezi la ugawaji wa kadi za bima ya afya bure likiendelea katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Rukwa ili kuwafikia walengwa wengi zaidi.
Mzindakaya amesisitiza kuwa mpango huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, zinazolenga kuboresha ustawi wa wananchi kwa kuhakikisha wanapata huduma bora za afya pamoja na fursa za kujikwamua kiuchumi.
Katika hatua nyingine Mzindakaya amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika mpango huo wa bima ya afya bure pamoja na kuanza kuunda vikundi vya ujasiriamali kwa ajili ya kupata mikopo ilioelekezwa kwa Wanawake na Vijana .
Hata hivyo Mpango huo umeanza kutekelezwa kwa kuwapatia kadi za bima ya afya bure wananchi wasiojiweza ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya katika jamii.





