Wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wametakiwa kufuata Kanuni na maadili ya kazi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mkuu wa Divisheni ya Utumishi katika Wizara hiyo, Bi Subira Mtumwa Haji, amesema hayo wakati wa mafunzo kwa Wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo huko Migombani Wilaya ya Mjini.

Amesema ni muhimu kwa wafanyakazi kuzingatia kanuni na maadili ya utumishi wa umma ili kuhakikisha kazi za wizara zinafanyika kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa taasisi na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Afisa TEHAMA kutoka Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Idrissa Ali Kassim, amewataka Wafanyakazi hao, kuwa makini katika kulinda faragha zao sambamba na kutumia mitandao vizuri.

Aidha amesisitiza kuacha kutumia mitandao ambayo haina ulinzi ili kujikinga na taarifa mbalimbali ikiwemo kudukuliwa taarifa zao binafsi na kuhatarisha usalama wa mtumiaji.

Nao Wafanyakazi wa Wizara hiyo, wameahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili yaweze kuleta tija kwao na Taifa kwa ujumla.