MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Iringa, Zainabu Mwamwindi, amesema ushirikiano uliopo kati ya viongozi wa UWT ngazi ya mkoa na wilaya umewezesha kufanikisha malengo mbalimbali waliyojiwekea katika kuwahudumia wananchi na makundi yenye uhitaji katika jamii.Mwamwindi ameyasema hayo wakati wa ziara ya viongozi wa UWT Mkoa wa Iringa katika kituo cha kulea watoto cha Safina Street Network kilichopo Manispaa ya Iringa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani.
Amesema kuwa viongozi wa UWT waliona ni muhimu kutembelea kituo hicho ili kuwasalimia watoto wanaolelewa hapo pamoja na kuwapongeza walezi wanaojitolea kuwalea watoto wanaotoka katika mazingira hatarishi.
Alisema kulea watoto wanaotoka katika mazingira magumu si kazi rahisi na kunahitaji moyo wa kujitoa na upendo mkubwa kwa jamii.
“Nianze kwa kuwashukuru sana walezi wa kituo hiki kwa kazi kubwa mnayoifanya. Kulea watoto hawa si kazi ndogo, inahitaji moyo wa upendo na kujitoa. Kwa niaba ya wanawake wenzangu wa UWT Mkoa wa Iringa, tunawapongeza sana kwa juhudi zenu,” alisema Mwamwindi.
Aliongeza kuwa kazi wanayoifanya walezi wa Safina Street Network ni wito kutoka kwa Mungu kwani si kila mtu anaweza kujitoa kuwalea watoto waliotoka katika maisha ya mtaani na kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida.
Mwamwindi alisema ziara yao imelenga pia kutambua vituo vinavyotoa huduma kwa watoto wenye uhitaji ambavyo wakati mwingine havina wadau au watu maalumu wa kuvishika mkono pale vinapokumbana na changamoto mbalimbali na kuwashika mkono kwa vitu mbalimbali kama mchele, sukari mafuta ya kupikia, sabuni na unga.
Alisema UWT itaendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kusaidia vituo vinavyolea watoto ili kuhakikisha wanapata malezi bora pamoja na elimu.
Kwa upande wake Mratibu wa Safina Street Network, Erica Luhwavi, alisema shirika hilo limekuwa likifanya kazi ya kuwahudumia watoto wanaoishi au waliowahi kuishi katika mazingira hatarishi hususan mitaani, na kuwasaidia kubadilisha maisha yao.
Alisema licha ya changamoto wanazokutana nazo, wamekuwa wakiona mafanikio makubwa kwani baadhi ya watoto waliokuwa wakihudumiwa na shirika hilo sasa wamebadilika na hata kufanya kazi ndani ya shirika hilo kama watumishi.
“Wakati mwingine watu hudhani watoto wa mtaani hawawezi kubadilika, lakini ukweli ni kwamba wanapopata malezi na msaada sahihi wanabadilika na kuwa watu bora hata kuliko wengine,” alisema Luhwavi.
Alisema Safina Street Network ina matawi katika mikoa mitano nchini ambayo ni Iringa, Dodoma, Singida, Morogoro na Dar es Salaam, na imekuwa ikitoa huduma mbalimbali ikiwemo kuwafikia watoto mitaani, kuwapatia ushauri nasaha, chakula, matibabu pamoja na kuwasaidia kurejea shuleni.
Alieleza kuwa shirika hilo pia lina makao ya mpito (shelter) kwa ajili ya watoto wanaookolewa kutoka mtaani ambapo hupatiwa malezi ya awali, ushauri wa kisaikolojia na maandalizi ya kurejea katika familia zao pale inapowezekana.
Alisema watoto ambao hawawezi kurejea katika familia zao kutokana na changamoto mbalimbali hupokelewa katika nyumba ya malezi ya kudumu ambapo hupatiwa elimu na malezi hadi wanapoweza kujitegemea.
Hata hivyo alitaja changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kuwa ni uhaba wa makazi ya kudumu kwa watoto hao kwani nyumba wanazotumia kwa sasa ni za kupanga na hazitoshelezi mahitaji ya watoto wanaohudumiwa.
Katika risala iliyosomwa na watoto na vijana wa Safina Street Network, walieleza kuwa shirika hilo lilianzishwa mwaka 2007 mkoani Iringa na mpaka sasa limefanikiwa kuwahudumia watoto na vijana wasiopungua 283 waliokuwa katika mazingira hatarishi.
Walisema kupitia huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo, baadhi ya watoto waliokuwa wakiishi mitaani wameweza kurejea shuleni, wengine kuendelea na masomo hadi vyuo vikuu na baadhi yao kupata ajira.
Watoto hao walitumia fursa hiyo kuomba serikali pamoja na wadau mbalimbali kuwasaidia katika upatikanaji wa makao ya kudumu kwa ajili ya malezi ya watoto hao pamoja na mahitaji muhimu kama chakula, elimu na matibabu.
Pia waliomba kusaidiwa kuendeleza kiwanja cha ekari tano kilichopo eneo la Kigonzile mkoani Iringa kwa ajili ya kujenga makao ya kudumu ya watoto na vijana wanaohudumiwa na shirika hilo.





