NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Wilaya ya Iringa Benjamin Sitta ametoa wito kwa wazazi, walimu na wadau wa michezo kuhakikisha kuwa hamasa ya michezo inaendelea kuimarika katika maeneo mbalimbali ya jamii, ikiwemo mashuleni na mitaani.
Amesema kuwa ili michezo iwe na mchango chanya kwa vijana na jamii nzima, ni muhimu kuwa na matukio ya mara kwa mara kama mabonanza pamoja na kuongeza ushiriki wa maafisa michezo katika maeneo yao badala ya kubaki ofisini.
Katika mazungumzo yake, amesisitiza umuhimu wa wazazi kushirikishwa kikamilifu katika kutoa elimu kuhusu faida za michezo kwa watoto.
Ameeleza kuwa michezo ni njia muhimu ya kukuza vipaji, kujenga nidhamu na kuwaandaa watoto kisaikolojia na kimwili. Kwa mujibu wake, elimu hii ikitolewa ipasavyo mashuleni, itasaidia kuongeza mapenzi ya michezo na kuboresha maandalizi ya vijana kuanzia ngazi za chini.
Aidha, ametoa mwito kwa wadau kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya michezo, hasa kwenye viwanja vya shule ambapo serikali inawajibika katika hilo.
 Ameeleza kuwa wakurugenzi wataelekezwa kuhakikisha angalau baadhi ya viwanja vinaboreshwa ili viwe na uwezo wa kutumiwa na wanafunzi pamoja na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani.
 Aliongeza kuwa wadau wanaojitolea kutengeneza miundombinu wameanza kuleta mabadiliko, akitoa mfano wa jitihada zinazofanyika eneo la Mawelewele ambako viwanja vinatengenezwa na kuwekwa katika hali inayoridhisha kwa matumizi ya jamii.
Mkuu huyo wa wilaya amebainisha kuwa mkakati wa kukuza vipaji unapaswa kuanzia ngazi za vijiji, mashuleni na kuendelea hadi vijana wanaoshiriki mashindano kama UMISHUMTA na UMISSETA.
 Lengo ni kuviibua vipaji mapema na kuvilea ili vipate nafasi ya kuonekana na kuandaliwa kitaalamu kupitia programu za serikali na wadau binafsi, ikiwemo academies za michezo.
Katika hatua nyingine, ametaja mpango kabambe wa mkoa wa Iringa wa kuwa na timu ya mkoa itakayoshiriki ligi za kitaifa. Ameeleza kuwa ndoto ni kuiona mkoa wa Iringa una timu ambayo inapanda kutoka ngazi ya chini hadi kucheza Ligi Kuu dhidi ya timu kongwe kama Yanga SC na Simba SC.
Amewasilisha mipango miwili; wa muda mfupi na wa muda mrefu, ambayo yote yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi.
Mwisho, amekubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na madiwani pamoja na wadau wengine kuhusu kuangalia uwezekano wa manispaa au halmashauri kununua timu kwa ushirikiano na wadau binafsi ili kuleta maendeleo ya michezo katika mkoa.
Ametoa wito kwa kila mdau kutumia nafasi aliyonayo kuhakikisha kuwa vijana wanapata mazingira bora ya kukuza na kuendeleza vipaji vyao vya michezo.
Akizungumza katika kikao hicho, mdau wa soka Eliud Mvella alitoa ushauri kwa uongozi wa timu na wadau wote wa michezo, akisisitiza umuhimu wa kukaa pamoja na kupitia upya mpango wa uendeshaji wa timu hiyo.
Alisema kuwa kutokana na mazingira ya soko la michezo na uwezo wa timu yenyewe, ni muhimu kufanya tathmini pana ili kuepuka makosa ya kimfumo yanayoweza kuathiri maendeleo.
Alimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa hatua alizochukua awali katika wilaya ya Kinondoni na kusisitiza kuwa uzoefu huo unaweza kusaidia kuboresha mifumo ya usimamizi ndani ya Halmashauri ya Manispaa.
Aidha, alieleza kuwa changamoto zilizopo, ikiwemo masuala ya kiutawala na kifedha, zinahitaji nguvu ya pamoja na uelewa wa kina, akiwataka viongozi wote kuhakikisha wanaimarisha utendaji ili kuipatia timu mwelekeo sahihi.