Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania kwa kushirikiana na Televisheni ya Taifa ya Iran, umetangaza kifo cha Ayatollah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Kiongozi Mkuu wa Iran, aliyeripotiwa kuuawa katika shambulio la pamoja lililodaiwa kufanywa na Marekani na Israel.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tukio hilo limetokea asubuhi ya Jumamosi, tarehe 28 Februari 2026, ndani ya Ofisi yake katika Makao ya Uongozi wa Taifa hilo wakati akiwa akitekeleza majukumu yake ya kila siku.
Taarifa ya Ubalozi imeeleza kuwa Kiongozi huyo, aliyemtaja kama mwanazuoni na mpiganaji mkubwa, alitumia maisha yake yote kuitumikia Iran na Uislamu, na kwamba kwa mujibu wa imani yao, ameuwawa kishahidi na ataunganishwa na mashahidi wengine watukufu.
“Wakati wa tukio hilo alikuwa akitekeleza majukumu yake ya kawaida kama ilivyo desturi yake. Shambulio hili la kinyama lililotokea katika saa za mapema za asubuhi limeweka wazi kile tulichokiita propaganda na upotoshaji wa kisaikolojia wa maadui, na linaonesha kuwa aliendelea kuwa mstari wa mbele katika kutekeleza wajibu wake kwa ujasiri na bila woga,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa Baraza la Mawaziri la Iran limetangaza siku 40 za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo hicho, sambamba na kufungwa kwa shughuli za umma kwa muda wa siku saba.
Mpaka sasa, hakujakuwa na taarifa ya ziada kutoka mataifa yanayotajwa kuhusika na shambulio hilo.




