Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga (katikati) pichani, baada ya kufunga msimu wa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala msimu wa 2025/2026 na kufungua msimu mpya wa 2026/2027, mkoani Simiyu.Kutoka kushoto wa pili n Mkuu waa Mkoa wa Simiyu , Anamringi Macha na wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala(WRRB), Asangye Bangu. Picha na Baltazar Mashaka
……..
NA BALTAZAR MASHAKA, SIMIYU
SERIKALI imeziagiza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), kuwa na mkakati wa kuwawezesha wakulima kuanzia uzalishaji, ukusanyaji hadi uuzaji ili kuleta tija na bei nzuri ya Mazao.
Pia, imetoa rai kwa wakulima na wafanyabiashara kuwa waaminifu na kuunga mkono Mfumo wa Stakabadhi za Ghalani kwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, mbegu, teknolojia, na masoko ya uhakika ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kulinda maslahi ya wakulima, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa nchi.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Februari 25, 2026 , mkoani Simyu, wakati wa kufunga msimu wa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa msimu wa 2025/2026 na kufungua msimu mpya wa 2026/2027.
Aidha ameiagiza, WRRB kutoa elimu na kuwahamasisha wakulima, wafanyabiashara, wasimamizi wa ghala, na wadau wengine muhimu kutumia mfumo huo ili kuongeza uelewa na kuboresha ushiriki wao pamoja na wale wenye maghala ambayo hayajakidhi vigezo ili wafanikiwe kutoa huduma bora na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa mfumo huo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha amesema kufunga na kufungua Msimu wa Mauzo ya Mazao mkoani humo, imekuwa chachu na hamasa kwa wananchi kwa kuwa wameelewa maana na faida za kuendelea kutumia mfumo huo.
Mkurugenzi wa WRRB, Asangye Bangu, amesema msimu wa 2025/2026 umerekodi mauzo ya zaidi ya tani milioni 1.1 za mazao, ikiwa ni ongezeko la asilimia kutoka msimu uliopita ambapo wakulima wamejipatia shilingi trilioni 2.4, huku korosho, mbaazi, na ufuta yakiongoza mauzo hayo.
Aidha, mfumo umeendelea kupanuka kutoka wilaya 65 hadi 114, huku idadi ya waweka mali ikipanda kutoka 224 hadi 788, hali iliyoziongezea halmashauri mapato ya ushuru kufikia shilingi bilioni 65, umezalisha ajira zaidi ya 11,430 rasmi na zisizo rasmi na kuongeza leseni za maghala kufikia 286.
Katika msimu wa 2026/2027, WRRB imelenga kuingiza sekta za mifugo, ngozi, na mwani kwenye mfumo wa stakabadhi za ghala na inahimiza sekta binafsi kuanzisha maghala bora yanayohamishika.
Nao baadhi ya watumiaji na wanufaika wa mfumo huo kwa kuuza mazao yao katika mnada kwa uwazi kwa bei nzuri na kupata fedha kwa wakati, mkoani Simiyu, Daud Mpina na Mariam Litwina, wameionba serikali kuendelea kuboresha mfumo huo ulete tija zaidi.sss
