Na John Walter-Manyara
Halmashauri ya Wilaya ya Babati imepata gari jipya kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa shughuli za utawala pamoja na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Akilitambulisha gari hilo leo katika kikao cha Timu ya Menejimenti ya Halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Bi. Anna Mbogo, amesema kuwa gari hilo limetolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji.
“Serikali Kuu imetuletea gari lenye namba ya usajili SM 44487 kwa ajili ya shughuli za utawala. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutupatia gari hili,” amesisitiza Bi. Mbogo.
Ameeleza kuwa ujio wa gari hilo umefika katika kipindi muafaka ambapo Halmashauri ina majukumu mengi ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo pamoja na shughuli mbalimbali za kiutawala, hivyo litasaidia kuongeza ufanisi na kuwahudumia wananchi kwa wakati.
Gari hilo linatarajiwa kuwa chachu katika kuboresha usimamizi wa miradi ya maendeleo na kuimarisha utendaji wa Halmashauri kwa ujumla.




