NA, DENIS MLOWE, IRINGA
MWENYEKITI wa UWT Mkoa wa Iringa, Bi. Zainabu Mwamwindi, ameongoza maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutoa wito wa kuendeleza umoja, amani na upendo kama nguzo kuu za maendeleo ya Taifa.
Akihutubia akinamama na wanachama wa UWT mkoa Iringa walioadhimisha Kimkoa katika kata ya Kihesa Bi. Mwamwindi alianza kwa kusisitiza umuhimu wa kuyapokea na kuyahifadhi moyoni maneno ya amani na upendo:
“Niseme tu mama Samia yupo safi. Tumechagua amani na upendo kwa maendeleo. Tukiyatamka haya, tuwe tunayasimamia na kuyaishi katika mioyo yetu.”
Amesema maadhimisho ya miaka 49 ya CCM yanathibitisha uimara wa chama hicho ambacho, kwa maelezo yake, “kimezaliwa nyuma” ya umri wake lakini kimeendelea kuwa nguzo ya maisha yake ya kisiasa:
“Mimi nimekulia ndani ya CCM, naiishi CCM, na naendelea kuipenda. Natamani siku zote chama hiki kiendelee kuwa kichanga chenye nguvu, kinacholeta matumaini Wanawake tunayo sababu ya kujivuna” alisema
Mwamwindi amewataka wanawake kujivunia mafanikio makubwa ambayo chama na serikali yameyaleta, hususan chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tunatimiza miaka 49 ya CCM tukiwa na Rais mwanamke. Tunayo kila sababu ya kumsemea na kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan.”
Amesema utendaji wa rais umeonekana wazi katika kila kona ya nchi:
“Kwa mwenye macho na masikio haambiwi ona wala sikia. Hakuna eneo ambalo halijaguswa na kazi za mama Miradi ya afya, miundombinu na huduma kwa wananchi” Alisema
Mwenyekiti huyo ameeleza kwa kina namna ambavyo serikali imewekeza kwenye sekta za afya, elimu na miundombinu, Ujenzi wa vituo vya afya na zahanati nyingi maboresho ya mawodi ya kinamama na watoto na Kuboresha huduma katika hospitali za mkoa na wilaya
“Leo hii huduma za kinamama zimepamba moto kwa sababu huduma zinapatikana kwa urahisi. Nikienda Hospitali ya Ipamb huduma zote zipo. Hospitali ya Mkoa kila kitu kipo. Mama Samia ametujengea mazingira salama.”
Akionyesha msisitizo mkubwa, Mwamwindi amesema anashangazwa na wanawake wanaoibeza kazi ya Rais Samia:
“Mama Samia ni mwanamke mwenzetu. Nimeshangaa sana mwanamke anayeweza kumsema vibaya. Mama anafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha Watanzania tunasonga mbele.”
Mwito kwa wanachama na wanawake
Katika hitimisho lake, Bi. Zainabu Mwamwindi ametoa mwito kwa wanawake wa UWT na wananchi wote kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais za Kuendeleza umoja, upendo na amani aidha kuilinda na kuinadi CCM kama chombo cha maendeleo
“Leo tunasherehekea miaka 49 ya chama chetu na tunasherehekea mafanikio, heshima na dira ya maendeleo. Wanawake tunatamba kwa sababu kazi zinaonekana.”





