| Wadau wa Madini Singida Wanufaika na Soko la Madini Wapongeza Mfumo wa Bei Elekezi za Kidigitali Mtaala mkutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mjiolojia Mbeleye David akizungumza na wateja wanaofika kuuza dhahabu zao. ……………………………. Na Mwandishi Wetu, Singida Wadau wa
sekta ya madini wakiwemo wachimbaji, wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini
mkoani Singida wamepongeza uwepo wa Soko la Madini Singida, wakisema limeleta
mapinduzi makubwa katika biashara ya madini kwa kuimarisha uwazi, haki na
ufanisi kupitia matumizi ya mfumo wa bei elekezi za kidigitali. Akizungumza
katika soko hilo, Mtaalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Singida, Mjiolojia Mbeleye David, amesema kuanzishwa kwa soko hilo kumeleta
tija kubwa kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini kwa kuweka mifumo
inayowalinda dhidi ya udanganyifu wa ubora wa dhahabu na unyonyaji wa bei. Amesema
kabla ya kuanzishwa kwa masoko ya madini, mkoa wa Singida ulikuwa unaratibu
kiasi kidogo cha uzalishaji, kati ya gramu 100 hadi 200 pekee, lakini kwa sasa
kupitia masoko hayo umefanikiwa kuratibu uzalishaji unaoanzia kilo 50 hadi 60
kwa wachimbaji wadogo, hali inayoonesha ongezeko la ufanisi na imani ya wadau
katika mfumo huo. David
ameeleza kuwa Serikali imeweka mfumo madhubuti wa bei elekezi unaolenga
kumlinda mchimbaji mdogo dhidi ya kupunjwa kwa kuuza madini kwa bei duni. Amesema soko hilo limewekewa mashine ya kisasa
ya X-Ray Fluorescence (XRF) kwa ajili ya kupima ubora wa dhahabu, hatua
inayohakikisha madini yanauzwa kwa kuzingatia viwango sahihi vya ubora na
thamani halisi. Ameongeza
kuwa, tofauti na awali ambapo bei elekezi ilitolewa kwa dhahabu ghafi pekee,
kwa sasa soko linatumia ubao wa kidigitali unaoonesha bei elekezi za madini
mbalimbali ikiwemo dhahabu, shaba na fedha, jambo lililoongeza uwazi na kuondoa
mianya ya udanganyifu katika biashara ya madini. “Teknolojia
hii imeongeza uwazi na kurahisisha shughuli za masoko ikiwemo uthaminishaji wa
madini na utoaji wa vibali vya kusafirisha madini ndani na nje ya nchi, ambazo
sasa zinafanyika kwa wepesi na kwa haraka zaidi,” amesema David. Kwa upande
wake, mfanyabiashara wa madini, Abubakari Omary, amesema pamoja na mafanikio
yaliyopo, elimu kuhusu matumizi ya bei elekezi inapaswa kuendelea kutolewa kwa
wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili kuepusha sintofahamu na migogoro
wakati wa kufanya biashara. “Elimu ni
msingi muhimu ili kila mdau aelewe haki na wajibu wake na kufanya biashara kwa
kuzingatia bei halisi ya soko,” amesema Omary. Aidha, wadau
wamepongeza mfumo mpya wa masoko ya madini unaowawezesha wachimbaji wasio na
leseni kujisajili na kuuza madini yao moja kwa moja katika masoko ya madini
bila kulazimika kutumia leseni ya mfanyabiashara, hatua ambayo imeondoa kikwazo
kikubwa kilichokuwepo awali. Kwa ujumla,
uwepo wa Soko la Madini Singida umetajwa kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya
sekta ya madini mkoani humo, kwa kuongeza uwazi na usalama wa biashara, pamoja
na kuongeza mapato ya serikali kupitia kudhibiti na kuzuia utoroshaji wa
madini. Mtaalam
kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mjiolojia Mbeleye David,
amesema kuanzishwa kwa soko hilo kumeleta tija kubwa kwa wachimbaji wadogo na
wafanyabiashara wa madini kwa kuweka mifumo inayowalinda dhidi ya udanganyifu
wa ubora wa dhahabu na unyonyaji wa bei. Mfanyabiashara
wa madini, Abubakari Omary, amesema pamoja na mafanikio yaliyopo, elimu kuhusu
matumizi ya bei elekezi inapaswa kuendelea kutolewa kwa wachimbaji na
wafanyabiashara wa madini ili kuepusha sintofahamu na migogoro wakati wa
kufanya biashara. |