Jengo la Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma
Na Muhidin Amri,Mbinga
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya Songea Mkoani Ruvuma wakiongozwa na Mwenyekiti wake Desderius Haule, wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji Joseph Kashushura na watumishi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri miradi ya maendeleo.
Wametoa pongezi hizo jana walipotembelea miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Bwalo Shule ya Sekondari ya Wasichana Mbinga na Zahanati katika kijiji cha Mihango.
Akizungumza kwa niaba ya Madiwani hao,Haule alimtaka Mkandarasi anayejenga Bwalo ahakikishe anakamilisha ujenzi huo kwa wakati kama yalivyo makubaliano yaliyopo kwenye mkataba.
“Mwambieni Mkandarasi amalize kazi hii kwa wakati iwapo atachelewesha hatutasita kuvunja mkataba naye ili tulete mkandarasi ambaye atakamilisha kazi hii haraka” alisema Haule.
Kwa mujibu wa Haule,Halmashauri ina miradi mingi inayohitaji kumalizwa,hivyo Halmashauri haitamvumilia fundi yeyote atakayechelewesha kazi za ujenzi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Mbinga
Naye, Katibu wa Afya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga George Mhina alisema kuwa, Zahanati ya Mihango iko hatua ya mwisho kukamilika kabla ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa eneo hilo.
Mhina,ameishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya Mbinga kwa kutoa fedha za kujenga na kuboresha huduma za afya ambazo zimesaidia sana wananchi kupata matibabu karibu na makazi yao.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Mary Makondo, amefunga mafunzo ya ukusanyaji mapato kwa kutumia mifumo ya kielektroniki, akisisitiza uwazi, ufanisi na uwajibikaji kama nguzo za maendeleo ya haraka.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wataalamu kutoka Halmashauri za mikoa ya Ruvuma na Njombe na wataalamu wa Sekretarieti ya Mkoa wa Ruvuma ambayo yamefanyika Wilayani Mbinga Mbinga.
Lengo kuu lilikuwa kuwajengea uwezo watendaji kutumia teknolojia za kisasa kuongeza mapato ya ndani na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo, Makondo amewahimiza washiriki kwenda kuyatekeleza maarifa waliyopata kwa vitendo, akisisitiza kuwa mifumo ya kielektroniki ni chachu ya maendeleo endelevu kwa halmashauri na wananchi.
Mafunzo hayo yameendeshwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Dodoma), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuboresha ukusanyaji na usimamizi wa mapato nchini.




