Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla akifungua mafunzo hayo leo jijini Arusha
Happy Lazaro ,Arusha .
Arusha .Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amewataka Mawakili na Wanasheria kuzingatia weledi na kusaidia jamii ikiwa ni sehemu ya kutimiza maono na ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan kwa vitendo .
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akimwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Juma Homera katika ufunguzi wa mafunzo ya Mawakili wa serikali kuhusu msaada wa kisheria.
Ambapo amesema , mkakati wa serikali wa kuwatumia Mawakili wake katika kutoa msaada wa kisheria katika masuala yasiyokuwa na mgongano wa maslahi.
CPA Makalla amesema kuwa lengo la kukutana kwa Wanasheria na Mawakili wa Serikali ni kujengewa uelewa wa pamoja katika kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi ni utekelezaji wa vitendo wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuweka tabasamu kwa wananchi kwa kuondoa changamoto zao.
Aidha amefafanua kuwa, SAMIA LEGAL AID inalenga kutoa msaada kisheria, kutoa elimu, utatuzi wa migogoro na kuunganisha serikali na wananchi.
“Niwasihi sana kutumia weledi wenu katika kuhudumia wananchi na zaidi tujenge utamaduni wa kujitolea kwa wananchi kwani huduma za msaada kisheria ni wito lakini pia yachukulieni kwa uzito mafunzo haya na mtoe maoni yatakayoboresha mfumo wa msaada wa kisheria kwani bado tuna idadi kubwa ya wananchi wenye uhitaji.” amesema CPA Makalla.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Franklin Jasson Rwezimula amesema katika mafunzo hayo ya siku tatu, watajengeana uwezo kuhusu huduma za msaada wa kisheria, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, ushughulikiaji wa mashauri ya ukatili wa kijinsia pamoja na miiko ya utekelezaji wa majukumu ya wanasheria hao.
Mkurugenzi wa Sheria TAMISEMI, Wakili Richard Odongo, amesema juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha changamoto za kisheria, hasa migogoro ya ardhi, zinapatiwa ufumbuzi kwa wananchi wa ngazi za chini.
Naye Wakili Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Tamariz Mndeme, amesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi wa utoaji wa msaada wa kisheria na kusaidia wananchi kupata haki kwa haraka na kwa usawa.

